Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: MCL yaanza kupasha uchaguzi mkuu leo

Video Archive
Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati Taifa likijiandaa kuchagua viongozi wa kipindi cha miaka mitano ijayo, kampuni ya Mwananchi Commucations Limited (MCL) itashiriki maandalizi hayo kwa kuwapa wasomaji habari mbalimbali za uchaguzi kuanzia wakati wa ukoloni hadi uchaguzi wa Oktoba mwaka huu kuanzia leo.

MCL, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na kumiliki chaneli ya MCL Digital, itakuletea habari kuhusu uchaguzi uliofanyika wakati wa ukoloni na baada ya uhuru, ukihusisha uchaguzi uliofanyika chini ya siasa za chama kimoja na baadaye vyama vingi.

“Ili wananchi waweze kufanya uamuzi, wanahitaji kupata taarifa na katika kundi hili ndipo sasa vyombo vya habari tunapoingia,” alisema mhariri mtendaji mkuu wa MCL, Bakari Machumu.

“Na wajibu wetu ni kuhakikisha tunatoa taarifa za uwazi, ukweli na usiwe na kuegemea upande wowote.”

Alisema kuanzia leo “tutaanza mfululizo za makala kuelekea uchaguzi mkuu kwa ajili ya kuwapitisha wasomaji wetu wa kada mbalimbali kabla ya uhuru na hata tulipopata uhuru, mifumo ya uchaguzi ilivyokuwa, chaguzi zilizopita, mafanikio tuliyopata na changamoto zilizopo”.

Alisema MCL itahakikisha wasomaji wanapata habari zisizo na upendeleo, zilizochambuliwa, zenye weledi, ubora na zitakazosaidia wananchi kupata taarifa kamilifu na hivyo kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi muda utakawadia.

Pia Soma

Advertisement
“Unapozungumzia wajibu, kama chombo cha habari, lazima kuwe na msingi wa kusimamia haya ili kutenda haki kwa wadau wote wapate taarifa kwa wakati,” alisema.

Alisema MCL, ambayo ni kampuni tanzu ya Nation Media Group (NMG), itahakikisha inatoa habari zinazozingatia haki kwa kutumia vitu vitatu.

“Mosi, tutaendelea kutumia sera yetu mama ya habari tuliyonayo na wafanyakazi wote wanayo na inatumika kwa kampuni zote za habari zinazofanya kazi chini ya NMG inayoonyesha nini cha kufanya, nini cha kutofanya kwa waandishi na watangazaji wetu,” alisema.

Kitu kingine, kwa mujibu wa Machumu, ni sera inayoongoza uandishi wa vyombo vya mitandaoni ambayo pia imeshagawiwa kwa kila mfanyakazi.

“Tatu, pamoja na hizo sera mbili tunazozitumia wakati wote, wakati wa uchaguzi ukifika tunakuwa na sera inayotuongoza inayoitwa Management of Op-ed Content and Election Coverage (usimamizi wa maudhui na uandishi wa habari za uchaguzi),” alisema Machumu.

“Lakini sera hii inachambuliwa ili kwenda na uwiano na nchi husika, Kenya watakuwa na hii nao wanaifanyia maboresho kidogo ili kwenda na mazingira na sisi tunaifanyia maboresho haya ili kwenda na mazingira kama sheria za Tanzania.

“Kwa hiyo hii sera ya namna ya kutoa taarifa za uchaguzi ina mambo mengi inayoelekeza waandishi wa habari, wahariri na watu wa matangazo ya namna gani yatakavyofanyiwa kazi.”

Alisema vitu hivyo vitawezesha vyombo vya MCL kutoa habari ambazo hazitaegemea upande wowote, zenye weledi na zinazopasha wananchi habari zote kuhusu uchaguzi.

“Msimamo wetu kama Mwananchi Communications Limited (MCL) hatutamuunga mkono mtu au chama chochote, isipokuwa jukumu letu ni kuchochea majadiliano yenye tija ili kuwe na mijadala yenye tija kuonyesha tunakwenda kupata ufumbuzi wa matatizo yetu,” alisema.

“Ajenda yetu ni kuwawezesha watu kuwa na mijadala itakayowapa ufahamu utakaowawezesha kufanya uamuzi sahihi utakapofika wakati wa uchaguzi wakijua wanafanya uamuzi wao wa miaka mitano ijayo.”

Ili kufanikisha suala hilo, MCL imeunda dawati la uchaguzi litakalosimamiwa na Lilian Timbuka.

Uchaguzi utakaofanyika Oktoba utakuwa wa 15 tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza mwaka 1958 uliohusisha vyama vingi vya siasa na uliofanyika wakati wa ukoloni.

Uchaguzi wa mwaka huu pia utakuwa wa 12 chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa baada ya wa kwanza kufanyika wakati wa ukoloni kabla ya siasa hizo za ushindani kufutwa na hivyo uchaguzi wa chama kimoja kutawala kuanzia mwaka 1965 hadi 1990. Tanzania iliamua kurejea katika siasa za vyama vingi mwaka 1992.

Kwa ujumla, Tanzania imeshafanya uchaguzi mara 14 zikiwamo mbili za mwaka 1958 na 1960 ambazo hazikuhusu kumchagua Rais, bali wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria.

Uchaguzi uliofanyika chini ya chama kimoja cha siasa ulikuwa mwaka 1965, 1970, 1975, 1980, 1985 na 1990 na chaguzi zilizofanyika chini ya mfumo wa vyama vingi ni sita; 1962, 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

Ni katika misingi hiyo, vyombo vya MCL vitaanza kuchapisha habari za matukio yaliyotamba katika kila uchaguzi ili kuwawezesha wasomaji kujua nchi ilikotoka na inakokwenda.

Mbali na habari za kihistoria kuhusu chaguzi hizo, MCL pia itachambua ilani za vyama za uchaguzi uliopita na unaokuja ili kujua viliweka kipaumbele katika mambo gani kulingana na mwelekeo wa dunia na hali ya nchi.

Pia MCL imefanya mahojiano na watu mbalimbali walioshiriki au kushuhudia chaguzi mbalimbali, mabadiliko ya mfumo, mazingira na sheria.

Chanzo: mwananchi.co.tz