Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Lissu aibua mjadala kila kona nchini

Video Archive
Tue, 2 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tundu Lissu ameibua mjadala kila kona kutoka kwa watu wa kada mbalimbali wakihoji uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kumvua ubunge.

Wakizungumza na Mwananchi, watu hao wamesema hoja zilizotolewa na Spika Ndugai hazina mashiko kwa sababu baadhi ya viongozi wa Serikali walikwenda hospitali kumuona mbunge huyo wa Singida Mashariki, mahakama inafahamu na iliamua kusitisha usikilizaji wa kesi zake.

Walishauri kuwa Spika ambaye ni kiongozi wa Bunge angeweza kumpigia simu ili kufahamu maendeleo yake.

Mjadala huo unatokana na Spika Ndugai kutangaza bungeni juzi kuwa ubunge wa Lissu umekoma baada ya kutoonekana bungeni tangu Septemba 7, 2017.

Siku hiyo mchana, Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana kabla ya kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na usiku wake kupelekwa Kenya kwa matibabu zaidi.

Juzi akitangaza uamuzi huo, Ndugai alisema mambo mawili yaliyosababisha Lissu kupoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge ni kutotoa taarifa kwake (Spika) aliko na kutoandika au kujaza fomu za maadili ambazo hujazwa na wabunge kila mwaka.

Habari zinazohusiana na hii

“Nimetumia kifungu cha 37 (iii) sura ya 343 ya sheria ya uchaguzi inayonitaka kumpa taarifa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiwa kuna jimbo ambalo liko wazi kwa mujibu wa sheria. Nimemwandikia barua mwenyekiti wa tume aendelee na hatua za kulijaza,” alisema Ndugai.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk Athuman Kihamia alipoulizwa uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa marudio kwa sasa ikiwa ni takribani mwaka mmoja umebaki kabla ya uchaguzi mkuu ujao, alisema watatoa taarifa rasmi wiki inayoanza kesho.

“Barua ya Bunge tumeipata lakini ilikuwa kipindi cha wikiendi, kwa hiyo tutaoa taarifa ya pamoja kwa umma, kwa hiyo tusubiri muda,” alisema Dk Kihamia.

Hata hivyo, tangazo la Ndugai bungeni limezua mijadala kila kona huku pia maswali mengi yakiulizwa, ambayo hata hivyo yalishindwa kupata majibu jana kutoka kwa Spika Ndugai ambaye licha ya kutafutwa mara kadhaa kupitia simu yake ya kiganjani hakupatikana.

Spika Ndugai alitangaza uamuzi huo wakati Lissu akiwa nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu baada ya risasi 16 kumpata mwilini.

Baada ya kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa Dodoma kabla ya usiku huohuo kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, Januari 6 mwaka jana alihamishiwa nchiniUbelgiji.

Askofu Bagonza

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza alitoa ujumbe kupitia akaunti yake ya Facebook akisema, kuna tofauti kati ya Bunge na Bonge. “Bunge huongozwa kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni, tamaduni za mabunge, mila na desturi nzuri, busara na hekima. kikikosekana kimoja hapo juu, linageuka kuwa bonge.”

Kiongozi huyo wa kiroho alisema, “maana yake, bonge linatisha, linaonea, linapendelea, linajichanganya, linahujumu, linajihujumu, linalipiza kisasi, linakera na halina utu wala huruma. Bunge letu siyo bonge. Mungu Ibariki Tanzania. Libariki Bunge letu. Liepushe na majaribu ya kuwa bonge.”

Familia ya Lissu

Kaka wa Lissu, Wakili Alute Mughwai alisema familia inasikitishwa na uamuzi wa Spika Ndugai japokuwa haikushangazwa kwa sababu ya majaribio kadhaa aliyokutana nayo mdogo wake.

“Desemba mwaka juzi Spika Ndugai alipoulizwa na wanahabari kwa nini hakwenda kumwona Lissu hospitalini Kenya, akajibu alisubiri uchaguzi wa urais Kenya umalizike lakini hakufanya hivyo hadi leo badala yake tumeona majaribio kadhaa.

“Mwaka huu kama utakumbuka lilifanyika jaribio la kumnyima mshahara wake, akapiga kelele wakasitisha (mpango huo), kwa hiyo hatushangai na uamuzi huo,” alisema mwanasheria huyo na kusisitiza kuwa watakwenda mahakamani.

Mwenyekiti Chadema Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza katika kikao cha ndani kilichofanyika Kanda ya Nyasa juzi alisema Chadema ipo tayari kupoteza viti vyote, lakini haitaacha kufanya kazi kwa ajili ya wananchi huku akiwataka wanachama wa chama hicho kutokuwa na mioyo ya visasi.

“Yaani Spika leo anamfukuza ubunge Tundu Lissu anafikiri tutalia, tunamwambia mheshimiwa Spika wacha Lissu chukua viti vyote hivi, nani ana shida na ubunge, tuna shida na wananchi.”

“Wanatupa sababu zaidi za kufanya kazi, vitu kama hivi haviwezi kutukatisha tamaa, vinatuimarisha katika dhamira yetu, tunafanyiwa uonevu mwingi ndani ya Bunge, tunafanyiwa visa vingi. Hivi visa havituvunji moyo, vinatuimarisha,” alisema.

Alisema, “hasira ya kufukuza wabunge wetu, hasira ya kutoheshimu mawazo yetu, ya kuondoa michango yetu tutaimaliza kwa kupeleka wabunge wengi, kuondoa wingi wa CCM ndani ya Bunge na kuiongoza Serikali ya nchi hii.”

Bashiru aitetea CCM

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali alisema CCM haihusiki kwa namna yoyote na uamuzi huo wa Spika Ndugai, akisema hawezi kuzuia watu kuwa na hisia tofauti na hiyo ndiyo siasa.

Dk Bashiru alipotakiwa kueleza labda uamuzi wa Spika kufuta ubunge huo unatokana na ushawishi wa chama ili kukisaidia kuchukua jimbo hilo, alisema: “Watu lazima wajadili wawe na mitazamo tofauti, inayokinzana, inayofanana, mimi siingii kwa watu hao. Mimi ni chama taasisi. Kuna majimbo hubaki wazi kwa vifo, kujiuzulu, kuondolewa kwa mujibu wa sheria au kubaki wazi kila baada ya miaka mitano. Si jambo jipya na imetokea kwa Spika huyo, Spika anasimamia sheria, sasa tunahusikaje hapo (CCM),” alisema.

Alisema kama kuna mashaka juu ya hilo, walalamikaji wafuate ufafanuzi bungeni na si CCM, akisema upande wao ni chama cha siasa, wakisubiri hatua gani zitafuata baada ya jimbo hilo kubakia wazi.

Maoni ya wengine

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe alishangazwa kusikia hoja za Spika Ndugai zilizochagiza uamuzi huo ilihali Mahakama yenyewe imeamua kutambua matibabu yake na kusitisha usikilizaji wa kesi zinazomhusu.

“Kama Mahakama imeona hivyo tangu alipopelekwa nje kwa matibabu Kenya na baadaye Ubelgiji na alikuwa anazunguka (ziara) kwa sababu daktari wake alimruhusu kufanya mazoezi, sasa hii itawapa shida mahakamani,” alisema Rungwe, mwenyekiti wa umoja wa vyama 10 vya upinzani.

Dk Richard Mbunda kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kinachoonekana nje ya uamuzi huo ni mkakati ya kumwondolea nguvu atakayokuwa nayo Lissu kutoka kwa wapiga kura wake na wananchi pindi atakaporejea (Septemba 7) mpango utakaokuwa kinyume chake.

Watetezi wa haki za binadamu

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Dk Rugemeleza Nshala alizungumza suala hilo kwa kifupi akisema, “Ni uamuzi unaosikitisha sana, nadhani inatosha kutumia neno hilo.”

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa alisema uamuzi dhidi ya Lissu ni kukosa ubinadamu kwani alikuwa miongoni mwa wabunge waliojituma kabla ya kupata matatizo.

“Hata Ndugai aliwahi kuugua, na sasa tunajua kuna wabunge wengi wanaumwa. Lissu angewezaje kuja kujaza fomu za maadili akiwa kwenye matibabu nje? sisi (THRDC) tunashauri atumie mawakili wake kwenda mahakamani kupinga uamuzi huo au akiona inafaa amwachie Mungu,” alisema.

Naye Ofisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Tito Magoti alisema ni jambo la ajabu, linaloshangaza katika uamuzi huo kwa kutumia hoja alizotoa Spika Ndugai. Kuhusu hoja ya kujaza fomu, Wakili Magoti alihoji ni wakati gani Lissu alitakiwa kuja fomu za maadili.

“Anawezaje wakati hayupo nchini, bado taarifa zake ni mgonjwa, halafu hawezi kuthibitisha anaposema hana taarifa (Spika Ndugai) kwa hiyo walitakiwa kuwa waadilifu na kutoa sababu nyingine,’’ alisema Wakili Magoti.

Chanzo: mwananchi.co.tz