Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Kikwete asimulia siri ya kuanzishwa kwa Sadc

Video Archive
Sat, 10 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema Arusha ndio chimbuko la kuanzishwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).

Kikwete, ambaye amewahi kushika nafasi kadhaa za uwaziri ikiwamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 10 alisema hayo jana alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake Masaki jijini Dar es Salaam.

Akisimulia historia ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo hatua kwa hatua, Kikwete alisema baada ya makoloni ya Ureno katika nchi za Afrika kuwa huru, ulianzishwa umoja wa nchi za mstari wa mbele ukiwa na wanachama wa nchi za Angola, Botswana, Msumbiji, Tanzania na Zambia chini ya uenyekiti wa Mwalimu Julius Nyerere.

Kikwete alisema shabaha ya umoja huo ilikuwa ni kuongeza nguvu ya kuzikomboa nchi tatu za kusini mwa Afrika ambazo zilikuwa hazijapata huru, miongoni mwa nchi hizo zilikuwa Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini.

Alisema pamoja na juhudi hizo, kazi haikuwa rahisi kwa kuwa kuna nchi zilikuwa muhimu kimkakati katika juhudi hizo ambazo ni Swaziland (Eswatini) na Lesotho ambazo uchumi wake ulikuwa unategemea Afrika Kusini.

Pia, nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Angola licha ya kuwamo kwenye mkakati huo, lakini uchumi wake ulikuwa unategemea Afrika Kusini. Akifafanua kuhusu nchi hizo kuitegemea Afrika Kusini kiuchumi, alisema wananchi wengi wa mataifa hayo walikuwa wamepata ajira kwenye migodi ya madini nchini humo.

Pia Soma

Pia, alisema makaburu wa Afrika Kusini waliendeleza vitendo vya ubaguzi na kuwafanyia vurugu wale walioonekana kuunga mkono juhudi za ukombozi, ikiwamo kusaidia vikundi vya waasi.

Alisema kuna wakati makaburu walikuja Dar es Salaam kutaka kulipua Daraja la Selander, lakini hawakufanikiwa na waliporudi kwao waliionya Tanzania kwamba kama wameweza kufika hapo, basi wanaweza kufanya lolote.

Kikwete alisema vurugu hizo za makaburu ziliwafanya viongozi wa nchi tano za mstari wa mbele kuamua kufikiria namna nyingine ya kuepuka vitendo hivyo.

Alisema ndipo Mei 1979, viongozi hao wa nchi za mstari wa mbele walipoamua kuwapa jukumu la kutafuta suluhu ya matatizo hayo mawaziri wao wa mambo ya nje.

Walipokutana, mawaziri hao waliona umuhimu wa kuwashirikisha mawaziri wa sekta ya uchumi na Agosti 1979, walikutana Arusha wakatoa mapendekezo yao yaliyofikishwa kwenye mkutano wa viongozi hao uliofanyika Aprili Mosi, 1980 Lusaka, Zambia.

Kikwete alisema mkutano huo ulitoka na azimio la Lusaka la ukombozi wa kiuchumi na ndipo ilipoanzishwa Sadcc, lengo lake likiwa ni kuchukua hatua za kutoitegemea kiuchumi Afrika Kusini na makao makuu yake yakawekwa Gaborone, Botswana na mwenyekiti wake akawa Rais wa Botswana kwa wakati huo, Seretse Khama.

Alisema mwenyekiti wa nchi za mstari wa mbele aliendelea kuwa Mwalimu Nyerere. Nchi zingine kama Zimbabwe na Namibia zilipopata uhuru zilijiunga na Sadcc na mwaka 1990 Nelson Mandela alipotoka gerezani, viongozi hao walianza kufikiria upya namna gani ya kushirikiana na Afrika Kusini waliyokuwa wameitenga kutokana na ubaguzi wa rangi.

Kikwete alisema viongozi hao walikutana tena mwaka 1992 kwa ajili ya mjadala wa kuibadili jumuiya hiyo kwa lengo la kuipokea Afrika Kusini kuwa mwanachama mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) ambayo iliundwa.

Alisema umoja huo mpya ulikuwa na malengo ya kujitegemea kiuchumi, ulinzi na usalama, kuondoa umaskini na kusaidia makundi yasiyojiweza.

Akizungumzia uenyekiti wa Sadc, alisema haukuwa wa mzunguko kama ilivyo sasa kwani baada ya Khama kufariki dunia, uongozi ulichukuliwa na Quett Masire ambaye alirithi urais wa Botswana.

Pia, uongozi wa nchi za mstari wa mbele baada ya Nyerere ulichukuliwa na Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Kikwete alisema baada ya Mandela kuchaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini mwaka 1994, viongozi wa Sadc waliamua kumpa uenyekiti alioushika kwa kipindi cha miaka mitatu na baada ya hapo, utaratibu wa mzunguko ukaanza.

Chanzo: mwananchi.co.tz