Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Kangi Lugola, Zitto Kabwe sasa ni jino kwa jino

Video Archive
Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kwamba ndani ya siku mbili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ajisalimishe polisi akisema ametoa kauli za uchochezi kwenye mkutano wa hadhara, limepingwa ikielezwa hana mamlaka ya kufanya hivyo.

Lugola amemtaka Zitto ambaye pia ni kiongozi wa ACT-Wazalendo kuripoti kwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi.

Zitto akizungumzia agizo hilo alisema, “waziri hana mamlaka hayo na haya ni matamko katika mkutano. Walete legal arrest warrant (hati ya kisheria ya kukamata mtu).”

Waziri Lugola alitoa agizo hilo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu wizara hiyo.

Mbali ya hilo, alisema Zitto alikaidi agizo la Serikali la kutaka wabunge kufanya mikutano ndani ya majimbo yao.

Lugola alisema mbunge huyo alikwenda kufanya mkutano katika Jimbo la Kilwa Kusini akiwa na mbunge wa jimbo hilo, Suleiman Bungara maarufu Bwege.

“Kuna baadhi ya Watanzania bado wanaendelea kutoa kauli za kichochezi na kutukana viongozi, pia wanakaidi agizo la Rais hasa wabunge wanaotoka eneo moja kwenda lingine kufanya mkutano kwenye majimbo yasiyo ya kwao,” alisema Lugola.

“Zitto Kabwe mahali popote alipo ajisalimishe kwa mkuu wa polisi wa Mkoa wa Lindi ili achukuliwe hatua stahiki. Endapo hatajisalimisha ndani ya siku mbili, nitamuelekeza mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ili popote alipo akamatwe,” alisema.

Lugola alisema, “nataka niwaambie Watanzania nimeshakemea jambo hili na chaguzi zote zinazoendelea na zijazo hakuna atakayepona kama ataendelea kutukana viongozi na kutoa lugha za kichochezi.”

Alimwagiza IGP Simon Sirro kumchukulia hatua mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilwa (OCD), kwa madai ya kushindwa kuchukua hatua mapema dhidi ya Zitto.

Julai 29, Zitto alialikwa kushiriki mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Garden ulioandaliwa na Bungara ambaye taarifa zinadai aliitwa juzi kuhojiwa na polisi.

Waziri hana mamlaka

Akizungumzia agizo la Lugola kwa Zitto, mwanasheria mkongwe nchini Profesa Abdallah Safari alisema waziri hahusiki na mambo hayo isipokuwa polisi pekee ndio wenye jukumu hilo.

“Kazi yake ni kuhakikisha sera za usalama zinatekelezeka. Kama amechukizwa angemwita kimyakimya si kutamka hadharani wakati wenye mamlaka hayo ni polisi kisheria. Jambo hili si la kwanza, alishawahi kufanyiwa Edward Lowassa na Freeman Mbowe,” alisema Profesa Safari.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana aliungana na Profesa Safari akisema mwenye jukumu hilo ni polisi ingawa waziri husika ana mamlaka makubwa.

Alisema hakuna mahali palipoandikwa mtu akitenda kosa la jinai, basi kiongozi wa kitaifa atoe amri ya kumtaka ajisalimishe polisi, bali kazi hiyo inafanywa na OCD (mkuu wa polisi wilaya) au RPC (kamanda wa polisi wa mkoa).

“Hata kama sheria inampa mamlaka, angetumia busara ya kumwita kimyakimya badala ya hadharani au angefanya kama ilivyo kwa Lugumi (Said) ambapo alimwagiza IGP Sirro ampeleke ofisini kwake,” alisema Dk Bana.

Chanzo: mwananchi.co.tz