Dar es Salaam. Unamjua Kiza Besigye. Huyu ni mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini Uganda ambaye ametajwa katika kitabu cha rekodi za dunia cha Guiness kama kiongozi aliyekamatwa na polisi mara nyingi zaidi duniani.
Taarifa ya kitabu hicho imeeleza kuwa Besigye amekamatwa mara 50 nchini Uganda, Jumatatu Januari 21, 2020 ndio ilikuwa siku ya mwisho kwa kiongozi huyo kukamatwa na polisi.
Rais huyo mstaafu wa chama cha Forum Democratic Change katika mara 50 alizokamatwa, asilimia 30 ilikuwa mwaka 2016 ambako alikamatwa mara 15.
Mara ya mwisho alikamatwa akiwa anajiandaa kuwahutubia wafuasi wake katika uwanja wa mpira wa Bugembe na kuwekwa rumande katika kituo cha Polisi cha Nalufenya.
Besigye ambaye kitaaluma ni daktari, ni ofisa mstaafu wa Jeshi la Uganda aliyewahi kufanya kazi na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni miaka kadhaa kabla ya kufarakana.
Mwaka 2000 alianzisha chama cha FDC na kugombea urais kwa takribani mara nne bila mafanikio, huku Museveni aliyeanza kuongoza nchi hiyo tangu mwaka 1986 akishinda.
Habari zinazohusiana na hii
Kiza Besigye alizaliwa Aprili 22, 1956 katika wilaya ya magharibi ya Rukingiri, akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto sita, baba yao alikuwa ni polisi. Wazazi wote wa Kiza Besigye walifariki dunia wakati akisoma sekondari.
Mikasa aliyopitia
Mwaka 1975, alikwenda jijini Kampala kusoma udaktari katika Chuo Kikuu cha Makerere.
Siku moja, akiwa na umri wa miaka 18 alikwenda hotelini kula chakula cha jioni, baada ya muda alikwenda chooni na kuamua kuzungumza na wanafunzi.
Wakati akizungumza mtu mmoja wa miraba minne alimnyanyua na kumzaba kibao usoni kilichompeleka sakafuni.
Besigye alinukuliwa akisema safari yake ya kwenda chooni iliishia hapo.
Vuguvugu la mabadiliko lilipoanza nchini Uganda, halikuwa na mafanikio makubwa katika uchaguzi wa mwaka 1980,uliomuweka madarakani Milton Obote.
Dk Besigye aliliambia gazeti la East African kuwa hakujiunga mara moja na Museveni alipoingia msituni lakini alikamatwa na kushikiliwa kwa miezi miwili katika hoteli ya Nile mwaka 1981, akituhumiwa kushirikiana na waasi na hivyo kuteswa.
Awa daktari wa Museveni
Dk Besigye alikimbilia Nairobi lakini mwaka 1982 alijiunga na Museveni msituni na kuwa daktari wake binafsi.
Mara chache hakushiriki vita mstari wa mbele, Dk Besigye alikuwa akipelekwa katika vikosi vilivyokuwa vikipambana na kuwatibu askari waliojeruhiwa.
Museveni alipoingia madarakani, Dk Besigye akiwa na umri wa miaka 29, aliteuliwa kuwa waziri wa nchi wa masuala ya ndani na pia kamisaa wa Taifa wa siasa.
Uteuzi huu uliwashtusha baadhi ya watu waliokuwa pamoja na Dk Besigye msituni kwa sababu hakuwa amehusishwa katika masuala ya kisiasa wakati wa vita.
Baadhi wanaamini kupanda haraka kwa Dk Besigye kulionekana kama tishio kwa rais na matokeo yake alipewa majukumu madogo katika miaka ya 1990.
Urais
Dk Besigye alipanda na kufikia cheo cha kanali jeshini lakini hakustaafu kazi ya jeshi hadi muda mfupi kabla ya uchaguzi wa mwaka 2001 alipoandika taarifa inayotuhumu chama cha National Resistance Movement kwa ukosefu wa demokrasia, ufisadi na kutokuwa na uwazi.
Miezi michache kabla ya uchaguzi, alijitosa na kugombea urais.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi na Museveni, alikwenda mahakamani kupinga matokeo kwa madai kuwa Serikali ilitumia nguvu, vitisho na ghasia lakini kesi yake ilitupiliwa mbali na yeye kukimbia nchi.