Dar es Salaam. Kikao cha kwanza cha Rais John Magufuli na viongozi wakuu wastaafu hakijaisha bila maoni ya wananchi, ambao wamesifu na kutaka utamaduni huo uendelezwe.
Katika maoni yao kwa Mwananchi, wengi walikuwa kama wanasema “hii ndio inayotakiwa” baada ya gazeti hili kutafuta maoni yao kuhusu kikao hicho cha aina yake kilichofanyika juzi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Marais wastaafu wa Muungano na Zanzibar, waliowahi kushika nafasi ya makamu wa rais, mawaziri wakuu, wanasheria wakuu wa zamani, majaji wastaafu na waliowahi kushika nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano walihudhuria kikao hicho ambacho Rais Magufuli aliwahakikishia kuwa atafanyia kazi kwa asilimia 100 mawazo yao kuhusu uendeshaji wa nchi.
Serikali ya Rais Magufuli ni ya tano tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961, wakati Kassim Majaliwa ni waziri mkuu wa kumi na moja.
Ukiacha viongozi ambao hawakuwa Dar es Salaam na ambao wametangulia mbele za haki, kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi 20, kwa mujibu wa taarifa zilizotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais.
“Ni jambo zuri na linalofurahisha kukutana, na inaonyesha Rais anashaurika,” alisema aliyewahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), John Seka.
“Lakini hatujui hasa walichozungumza behind the scene (nyuma ya pazia) na baada ya hapo kipi kitafuata na kama anaweza kukifanyia kazi mimi na wewe hatufahamu.”
Lakini katika video iliyotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano, Rais ameahidi kufanyia kazi kwa asilimia 100 maoni ya wastaafu hao kuhusu uendeshaji nchi.
Sifa nyingine zilitolewa na Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), aliyesema kitendo hicho kinafaa kuwa endelevu.
“Ni tukio linalounganisha Taifa kwa sababu huyu Rais (Magufuli) aliyepo, anajenga sehemu iliyokwisha anza kujengwa na hao waliomtangulia,” alisema Askofu Bagonza.
“Ni hatari, na narudia tena ni hatari kwa kiongozi kudhani kwamba yeye ndiye anayeanza kujenga nyumba, jambo ambalo si sahihi na kwa hiyo kitendo hicho cha kukutana ni kizuri sana.”
Hoja ya Askofu Bagonza inalingana na ya mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Nguruma.
“Ni jambo jema ambalo linapaswa kuungwa mkono na kila mtu,” alisema ole Nguruma.
“Isiwe hao viongozi wanasubiri kuitwa tu, bali kuwe na jukwaa la wazee ambalo litatumika kushauri viongozi walioko madarakani wanapokosea. Wamwite Rais wakati wowote ili kumpa ushauri.”
Lakini katibu wa Baraza la Wazee la Chadema, Roderick Lutembeka alisema kitendo cha Rais Magufuli ni kusikiliza kilio chao cha muda mrefu.
“Sijui lengo la Rais, lakini binafsi na hata kama umefuatilia mikutano yetu na waandishi wa habari tulikuwa tukimsihi mara kwa mara akutane na makundi ya watu katika jamii awasikilize kwa sababu hii nchi haiwezi kuongozwa na mtu mmoja tu,” alisema Lutembeka.
“Rais mwenyewe alishasema hawezi kujifungia ndani na kufanya kila kitu mwenyewe. Naamini kama ataendelea hivyo kwa kukutana na makundi mbalimbali nchi yetu itatoka kwenye mkwamo huu tuliomo.”
Akizungumzia mkutano huo, Rais Magufuli alisema amewaita wastaafu hao ili kujadiliana nao kwa kuwa wao ni viongozi muhimu na kwa nyakati tofauti walitoa mchango mkubwa katika Taifa.
“Nina bahati kuwa kiongozi wakati viongozi wengi wakiwa bado hai,” alisema.
“Ni sehemu chache duniani kuwa kiongozi halafu wale waliokutangulia wakiwa bado wapo. Nashukuru sana.”
Viongozi waliohudhuria ni marais wastaafu wawili wa Muungano; Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, Amani Abeid Karume (Zanzibar) na Mohammed Gharib Bilal aliyekuwa makamu wa Rais wa Muungano.
Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu saba; Dk Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba, Cleopa Msuya, John Malecela, Edward Lowassa, Frederick Sumaye na Mizengo Pinda.
Pia walikuwapo maspika wastaafu; Pius Msekwa, Anne Makinda na wa sasa Job Ndugai, huku waliowahi kushika nafasi ya Jaji Mkuu wakiwa ni Barnabas Samatta, Augustine Ramadhani na Othman Chande.
Kwa mujibu wa video zilizotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, viongozi hao walipewa nafasi ya kuzungumza kuhusu mwenendo wa nchi na walikuwa na maoni tofauti; kuanzia kupongeza hatua zilizochukuliwa hadi kukosoa baadhi ya maamuzi.
“Serikali inafanya vizuri na mwelekeo ni mzuri,” alisema Jaji Warioba, lakini akatahadharisha.
“Wakati mnapitisha sheria ya madini, mimi nilikuwa kijijini, lakini wakanitafutia ile miswada, nikaisoma na nikabaini changamoto. Nikampelekea ujumbe kwa Profesa Kabudi, Dodoma,” alisema.
“Nikamwambia Waziri naona mwelekeo wa sheria hizi, unarudisha juhudi za taifa za kuandaa mipango yake. Mipango ina hangover, lakini mjitahidi kuona mambo yanayoweza kutukwamisha hapa ndani na ya nje.”
Naye Mwinyi, ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Pili, alisema nidhamu ya kazi imerudi maofisini ambako watu wanalipwa kwa kufanya kazi na si kwa kwenda ofisini.
Mwinyi, ambaye anasifika kwa kurejesha siasa za ushindani na kurudisha uchumi huru, alisema kinachoendelea kimefanya watu watambue kuwa kuna Serikali na hivyo kuwezesha kila mtu kujua kinachofanyika.
Lowassa, ambaye alijiunga na upinzani wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alizungumzia umuhimu wa kutoa kauli kwa uangalifu ili kulinda amani.
Alisema jambo la pili ni ushauri wa kujengwa taasisi ili zidumishe hali hii ili wakati wote watu wajue kuna Serikali.
Inaonekana suala la ujenzi wa taasisi lilizungumzwa kwa kirefu katika kikao hicho na Mwinyi alionyesha hilo katika maoni yake.
“Naona ni jambo jema kama wenzangu wengi walivyozungumzia kuwe na taasisi kama zinahitajika,” alisema rais huyo mstaafu.
“Kama hazipo zijengwe, ili zidumishe hali hii. Wakati wote watu wajue kuwa kuna Serikali. Lakini kwa ujumla nataka na ninaomba, Serikali iendelee kufanya kazi na kila mmoja aone kama hii ni Serikali.”
Lowassa, ambaye alikuwa mmoja wa mawaziri wakuu katika Serikali ya Awamu ya Nne, alizungumzia amani na kusisitiza kuwa maneno yasiyopimwa yanaweza kuiondoa.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa, ukitaka kupima nchi yenye amani na demokrasia, hesabu viongozi wako walio nje, kwa sababu wengi watakuwa wametoroka. Lakini hapa tuna amani, ndiyo maana wengi wapo,” alisema.
“Lakini ni kwa kiasi gani tunaitunza hiyo amani, ni kwa kauli zetu na vitendo vyetu.”
Suala la chuki lilizungumzwa na Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu.
“Kama mtakumbuka nilichosema wakati nahamia upinzani, nilisema sina chuki na CCM na Rais Magufuli au na Rais (wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete, lakini nilisema kuwa kwenda huko ni kwa faida ya CCM,” alisema Sumaye ambaye sasa ni mwanachama wa Chadema.
“Ninajua ninachokifanya na nina hakika mngekuwa mnajua juhudi tunazoweka upande wa pili, mngesema tunafanya kazi nzuri kwa ajili ya nchi hii. Kwa hiyo nataka tu niseme hakuna uadui wowote.”
Hata waliozungumza na Mwananchi jana walikuwa na maoni kwa Rais Magufuli kuhusu kikao hicho.
“Lisiwe suala la sasa au kushtukiza, linatakiwa kuwa endelevu na lenye uwazi na si kificho,” alisema Askofu Bagonza wa KKKT.
“Wanapaswa kuwa wanaonana mara kwa mara na ikiwezekana kuwa sehemu za tunu za Taifa.” Naye Ole Nguruma alisema Rais asiishie katika kukutana na kundi moja la viongozi wastaafu, bali aongeze wigo.
“Rais amechaguliwa na wananchi wa makundi mbalimbali, asiishie kwa viongozi wastaafu tu, bali pia makundi mengine kama kiongozi wa dini, siasa na mengineyo,” alisema kiongozi huyo wa THRDC
“Ni sawa na kujiangalia kwenye kioo kisha unajirekebisha. Lazima taasisi kubwa kama Ikulu iongozwe na maoni ya wananchi walioiweka Serikali madarakani.
“Hawezi kuwaita wananchi wote Ikulu, ndiyo maana anaita kwa makundi. Aendelee kuwaita na kusikiliza maoni yao na kuyafanyia kazi.”