Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Dk Kigwangalla anavyomkumbuka Ruge kwa Tanzania Unforgettable

Video Archive
Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema aliyekuwa mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba alikuwa mgonjwa lakini alishiriki kikamilifu kuiandaa Tanzania Unforgettable

Akizungumza nyumbani kwake jijini Dar es Salaam katika mazungumzo maalum na Mwananchi leo Jumatano Februari 27, 2019, Dk Kigwangalla amesema Ruge alikuwa mtu mashuhuri hapa nchini na Taifa liko kwenye majonzi makubwa.

“Ni mtu ambaye alijijengea jina kubwa katika tasnia ya habari, maendeleo, uchumi na burudani kwa ujumla,” amesema.

Amesema heshima hiyo ameipata kutokana na uwezo wake wa kubuni vitu mbalimbali na wengine wamediriki kusema yeye ndiye alikuwa injini ya Clouds kwa kuwa anazalisha vitu siku hadi siku.

Dk Kigwangalla amesema Ruge alikuwa mkali kwa vijana wanaochipukia na wale ambao walikuwa hawafuati maelekezo hawakuelewana.

“Ni mtu ambaye ameweza kufanikiwa kutokana na kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na watu na ni mtu ambaye alikuwa anaheshimu sana mamlaka,” amesema.

Waziri huyo amesema Ruge aliweza kufanya kazi za Serikali hasa pale alipomteua kuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati ya kuandaa utambulisho mpya wa Tanzania na mwisho ikapatikana kauli mbiu ya ‘Tanzania Unforgettable.’

Amesema hata vijana wa kubuni kauli mbiu hiyo aliwapeleka Ruge. “Ruge alifanya kazi kwa bidii usiku na mchana huku yeye akiwa anaumwa,” amesema.

“Siku moja kabla ya mimi kupata ajali (Agosti 3,2018), tulikuwa Arusha na licha ya yeye kuwa India anaumwa lakini aliporejea nchini hata kabla hajaripoti kazini kwake alikuja Arusha na alishiriki kikamilifu.

“Ruge alikuwa mtetezi sana wa hoja mbalimbali zilizotolewa na wadau wa utalii, alijitoa sana kwa kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na wadau na kwa kiasi kikubwa ‘Tanzania Unforgettable’ ameishiriki kikamilifu,” amesema Waziri Kigwangalla

Akifafanua kuhusu Tanzania Unforgettable alisema ni mahali mtu akija kutembelea, uzoefu atakaoupata hauwezi kuisahau nchi ya Tanzania, akitembea ufukweni, Mlima Kilimanjaro na kila kitu kinampa mtu uzoefu ambao hawezi kuusahau.

“Kwa vyovyote vile nchi yetu imebarikiwa sana kuwa na vijana wenye vipaji hivyo Watanzania wanapaswa kujivunia sana kuzaliwa Tanzania na mimi sisemi sana kwa kuwa Ruge amefariki lakini ni kweli Ruge alikuwa mtu muhimu sana,” amesema.

Soma Zaidi: VIDEO: Mwili wa Ruge kuwasili Ijumaa, kuzikwa Bukoba Jumatatu

Kupata mahojiano zaidi kati ya Mwananchi na Dk Kigwangalla usikose gazeti lako la Mwananchi kesho Alhamisi Februari 28,2019



Chanzo: mwananchi.co.tz