Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: DPP asimulia dhahabu, fedha zilizotoroshwa Kenya zilivyopatikana

Video Archive
Wed, 24 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amesema ushirikiano kati ya ofisi yake na ya DPP wa Kenya imefanikisha kurudishwa Tanzania kwa kilo 35.34 za dhahabu na fedha vilivyotoroshwa kwenda Kenya tangu mwaka 2004.

Akizungumza leo Jumatano Julai 24, 2019  katika hafla fupi ya makabidhiano hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Mganga amesema utaratibu wa kurejeshwa kwa dhahabu hizo ulianza tangu Rais Magufuli alipokuwa mapumzikoni wilayani Chato, mkoani Geita.

“Februari 15, 2018 dhahabu ya kilo 35.34 ilikamatwa katika uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta wakati msafiri mmoja (anamtaja) aliyekuwa akisafiri kwa ndege ya Presission Air kutoka Mwanza alikamatwa,” amesema Mganga.

Amesema baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa Wakurugenzi wa Upelelezi wa Kenya na Tanzania walianza upelelezi, aliongoza timu ya watu 11 kuhakikisha dhahabu hiyo inarejeshwa.

Mbali na timu hiyo, Mganga amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali  (AG), Profesa Adelardus Kilangi aliandika maombi kwenda Kenya kuhakikisha dhahabu hiyo irejeshwe na kutumika kama kielelezo cha kesi.

Amesema kesi hiyo namba 8 ya 2018 ya uhujumu uchumi imefunguliwa jijini Mwanza.

Pia Soma

“Tulipofika nchini Kenya tuliongea kwa undani na ndugu yangu Rubin Haji (DPP- Kenya) na viongozi wengine kuhakikisha dhahabu hiyo inarudi,” amesema.

Mbali na dhahabu hiyo, DPP Mganga amesema leo pia wanapokea fedha zilizoporwa mwaka 2004 na mtuhumiwa kukimbilia Kenya.

“Ilitokea tarehe 21, 3 mwaka 2004 wakati benki ya NBC tawi la Moshi ilipovamiwa na watu wakawakamata watu walio ndani, ilikuwa saa 9 mchana siku ya Ijumaa,” amesema Mganga.

Amebainisha kuwa taratibu za kumrejesha nchini zilikuwa zimeshindikana miaka yote, lakini kwa ushirikiano kati yake na DPP wa Kenya,  mshtakiwa huyo amesharejeshwa Tanzania na kesi yake iko Moshi.

“Tulikuwa tunasubiri ushahidi wa vielelezo alivyokamatwa navyo ni Sh170 milioni za Tanzania, Dola 77,500,  fedha za Kenya Sh171,600 vyote hivi naimani ataturejeshea ili kesi iweze kuendelea,” amesema Mganga.

Chanzo: mwananchi.co.tz