Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali Charles Kichere amesema anaingia kwenye ofisi hiyo akiwa amejipanga kikamilifu kulinda mapato yanayokusanywa.
Akizungumza leo wakati anakabidhiwa ofisi amesema atasimamia kwa kikamilifu kuhakikisha anaangalia mapato hayo yanatumikaje ili kuwaletea ustawi watanzania.
“Nimefanya kazi TRA najua ugumu wa kukusanya mapato. Nitayalinda mapato kwa wivu mkubwa, sitakuwa na simile kwa wanaotumia vibaya mapato ya serikali nitawaripoti ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,”
“Nitafanya kazi hii kwa kuzingatia weledi na uadilifu kama alivyosema Profesa CAG kazi yake ni kuchukua jukumu la kuweka saini. Ripoti inaanzia chini kabisa hivyo kazi kubwa inafanyika chini, nitashirikiana nao.
Nitajenga timu nzuri kuhakikisha kuanzia chini kunakuwa na timu nzuri, huwezi kufanya kazi na watu wakiwa wamesambaratika hapo utakuwa umesambaratisha taasisi na nina uhakika hautafurahi kuona mwanafunzi anafanya hivyo,”