Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi waombwa kumbukumbu ya Mfugale

Faf002c25a7eee9b4c7cce544b4d1edf.jpeg Ujenzi waombwa kumbukumbu ya Mfugale

Fri, 2 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi imeombwa kutafuta namna ya kujenga kumbukumbu ya kudumu ya aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Patrick Mfugale, kutokana na mchango mkubwa aliotoa katika taifa kwenye ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Mfugale (68) aliyefariki dunia ghafla juzi jijini hapa, mwili wake uliagwa jana katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alikofariki, na kusafirishwa jana jioni kwenda mkoani Dar es Salaam utakapoagwa leo kuanzia asubuhi.

Akitoa salamu za Bunge akimwakilisha Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso aliitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kutafuta namna ya kuweka kumbukumbu kuenzi mchango wa mhandisi Mfugale.

“Tutafute kitu cha kumuenzi kama kumbukumbu ya kudumu, kila mahali amefanya kazi. Niiombe wizara kutafuta kitu kingine kwa ajili ya kumbukumbu ya kudumu, hata kama kuna kumbukumbu ya liile jina la Daraja la Mfugale kule Dar es Salaam…bado haitoshi kwani amefanya mambo mengi sana katika nchi hii,” alisema Kakoso.

Alisema Mfugale alikuwa kielelezo kwa taasisi ya Bunge, na kila mbunge na serikali anafahamu kazi alizofanya. “Spika kanituma nije nitoe pole kea wahandisi wote hapa nchini waliofanya kazi naye. Alikuwa mpole, anayejishusha, anayejali, na alifanya kazi mpaka siku ya mwisho,” alisema Mbunge huyo wa Mpanda Vijijini mkoani Katavi.

Alisema Mfugale alikuwa Mwenyekiti wa miradi mikubwa inayojengewa nchini na alikuwa anasimamia ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Pia alisimamia na kubuni miradi ya ujenzi wa madaraja ya Kikwete mto Malagarasi, Daraja la mto Kilombero, Daraja la Rusumo, Daraja la Mkapa, Daraja la Kigongo Busisi, Daraja la Kigamboni na Daraja la Tanzanite.

“Tumempoteza mtu muhimu sana katika Taifa, atakumbuka na Watanzania wote na Mkoa wa Iringa alikotoka, serikali ipo pamoja na wafiwa. Kadri wasifu wa mtu unapokuwa mzuri ni dalili kuwa aliwatendea mema Watanzania, yale madaraja na barabara zikitumika vyema ni ibada ambayo itakumbukwa, tumuombee kwa Mungu amsamehe makosa yake aliyoyafanya,” alisema Kakoso.

Aliwataka watendaji wa wizara na Tanroads kuendeleza miradi aliyoiacha Mfugale ambayo alishabuni mradi wa ujenzi wa barabara za mzunguko na Uwanja wa Michezo jijini Dodoma na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma.

“Pengo lake ni vigumu kuliziba, walioachiwa nafasi yake wayaendeleze,” alisema.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alisema Mfugale alikuwa ni kamusi ya miundombinu, mwalimu, mzalendo na mwadilifu.

“Katika Biblia kwenye Petro 4:12-13 tunaambiwa tusifadhaike kwa sababu ameshamaliza kazi yake,” alisema.

“Aliyofanya Mfugale kwenye nchi hii ni mengi sana, lakini sasa amelala na hakuna anayeweza kumuamsha, lakini tunapaswa kuendeleza yake mazuri ambayo ameyaacha,” aliongeza.

Mdogo wa marehemu, Richard Mfugale alisema kaka yake alianza kazi mwaka 1976 na amefariki akiwa na miaka 68.

“Tunaishukuru wizara walimuamini wakampa nafasi ya kusimamia wenzake, alikuwa na karama ya uongozi na akaionesha karama hiyo. Ameitumikia Wizara ya Ujenzi na ameleta matunda yanayoonekana kwa taifa, kama familia tumefarijika sana,” alisema Richard.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika alitoa pole na kusema wauguzi waliompokea Mfugale hospitalini hapo walifanya kazi kubwa.

“Tulimpokea siku ya Jumanne na wauguzi walifanya kazi kubwa sana, lakini juhudi zilishindikana kwani kazi ya Mungu haina makosa,” alisema Dk Chandika.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka alisema Jumatatu alimpokea uwanja wa ndege na amekuwa rafiki yake kwa miaka 12. “Nilipompokea nikamsindikiza kwenye gari nikamfungulia mlango wa gari akasema kufunguliwa mlango wa gari na RC ni heshima kubwa sana, tukapanga tupate chakula cha pamoja, lakini haikuwezekana kutokana na baadhi ya wenzetu tuliopanga kuwa nao kupata udhuru,” alisema Mtaka.

Chanzo: www.habarileo.co.tz