Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHUNGUZI WA MIKATABA: Kangi Lugola hapumui - VIDEO

Video Archive
Fri, 31 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma/Serengeti. Si bungeni, si mkoani kwake, si serikalini au si katika ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kote huko Kangi Lugola yuko katika hali ngumu.

Tangu uteuzi wa Lugola kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ulipotenguliwa na Rais John Magufuli Januari 23 kutokana na mkataba wa Sh1 trilioni ambao Rais alisema “wa hovyo”, amekuwa akijikuta katika tatizo moja baada ya jingine.

Mkataba huo ni kati ya Jeshi la Zimamoto na Ukoaji na moja ya kampuni ya Romania na ulilenga, pamoja na mambo mengine, kununua vifaa vya jeshi hilo.

Lakini Rais alisema mkataba huo haukufuata taratibu za manunuzi na haukupitishwa na vyombo husika kama Bunge, na hivyo kutengua uteuzi wa Lugola pamoja na Thobias Andengenye, aliyekuwa kamishna jenerali wa Zimamoto na Uokoaji.

Pia aliridhia barua ya Brigedia Jenerali Jacob Kingu ya kujiuzulu nafasi ya katibu mkuu wa wizara hiyo na kuagiza Takukuru ichunguze sakata hilo.

Mbunge huyo wa Mwibara alijikuta katika hali ngumu juzi wakati Kamati ya PAC ikiwasilisha ripoti yake ilimtaja katika sakata la hati za kusafiria za kielektroniki.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Mkoani kwake, Mara, CCM inamsubiri kumhoji baada ya kupata taarifa za kutimuliwa kwa Lugola kutokana na mkataba wa ufisadi huku akipata wakati mgumu wakati wabunge wakichangia mjadala wa ripoti ya PAC.

Juzi, kaimu mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo aliambia Mwananchi juzi kuwa leo wataanza kwa kumhoji Lugola kisha wengine wote waliotajwa ili kupata ukweli wa nyaraka walizonazo na baada ya hapo hatua zitafuata.

Lugola amehojiwa leo  January 31 katika ofisi za Takukuru zilizopo Dodoma, huku akijiandaa kwa mahojiano na chama chake mkoani Mara baada ya mkutano wa sasa wa wiki mbili wa Bunge kumalizika.

“Tunayo sababu na mamlaka ya kumuita na kumhoji kwa sababu ni mbunge anayetokana na CCM na jimbo lake liko ndani ya mkoa wa Mara,” alisema mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Samwel Kiboye maarufu kwa jina la Namba Tatu

“Ni vikao vya CCM mkoa ndivyo vilivyomjadili na kupendekeza jina lake kwa ajili ya uteuzi kugombea nafasi ya ubunge uliompatia sifa ya kuteuliwa kuwa waziri.”

Alisema vitendo vinavyodaiwa kutendwa na mbunge huyo si tu vimemfedhehesha Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, bali pia vimewafedhehesha wajumbe wa vikao vya kimaamuzi waliomjadili na kupendekeza jina lake katika nafasi ya ubunge.

“Ataitwa lini, kikao kitafanyika wapi na tuhuma zipi tutamtaka ajibu linabaki kuwa suala la ndani ya chama ambalo hatulianiki katika vyombo vya habari. Ninachoweza kuthibitisha ni kweli tutamuita na kumhoji,” alisema Kiboye.

“CCM Mara tutawadhibiti na kuwachukulia hatua wanachama na viongozi wote watakaokiuka maadili na kukifedhehesha chama kwa namna yoyote, iwe ndani au nje ya mkoa.”

Ilichokibaini PAC

Lakini hali ilikuwa ngumu bungeni juzi wakati watunga sheria walipomuweka kati ofisa huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi kuhusu mikataba waliyosema ya kifisadi katika wizara hiyo aliyoiongoza kwa siku 571 kuanzia Julai 1 mwaka 2018.

Wabunge hao, hasa wa upinzani, walizungumzia suala la hati za kusafiria za kielektroniki (e immigration), sare za polisi na mkataba huo wa Zimamoto uliosababisha kutenguliwa kwake, huku Naibu Spika Tulia Ackson akiwarejesha wabunge katika mstari.

Mmoja wa wabunge hao ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka.

“Ninachoweza kusema, kama mwenyekiti, kwanza tuna mkataba huu wa e-immigration. Kamati ilikaa na ikaomba Serikali ilete ule mkataba ili iweze kuufanyia kazi,” alisema mwenyekiti huyo.

“Badala ya ofisa masuhuli kuuleta, tukapata maelezo ambayo barua sina haja ya kuisoma hapa kwamba kamati tulimalize tu maana lina mambo nyeti.”

Alisema kitu kilichomshangaza ni maandishi ya maelekezo hayo hayaonyeshi kwamba kuna weledi, akisema wahusika hawaelewi kwamba kamati inafanya kazi kutokana na taratibu zilizowekwa na Bunge.

“Kamati haina mamlaka ya kufuta hoja yoyote ya (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) CAG kama hoja haikuletewa vielelezo au kama CAG hakukubaliana na maelezo,” alisema.

“Niliongea na Spika kuwa kazi aliyotupa ni kufuata taratibu za Bunge na fedha yote ya umma lazima itolewe maelezo na jinsi manunuzi yaliyofanyika kama yamefuatwa.”

Alisema mapato yanayotokana na e passport yawiane na uwekezaji uliofanyika, lakini akahisi kuwa Rais hakushauriwa vizuri. Alisema ndio maana Rais alipogundua yaliyotokea kwa Lugola alimsimamisha na kumuwajibisha na kwamba kama ni hivyo wanategemea hilo la e-immigration.

Hata hivyo, alisema suala hilo bado halijaisha na kwamba wanalifanyia kazi pamoja na CAG ili utaratibu ufuatwe.

“Kama kuna jambo lolote Rais akae na Spika ili amueleze tatizo, aweze kumshauri kutokana na sheria za kibunge. Ili kuanzia hapo sisi tunaweza kukaa na kusema jambo hilo limefungwa ama bado,” alisema.

Alisema wao pia walihusishwa na sakata la sare za polisi na yeye akiwa Afrika Kusini, wenzake waliteuliwa pamoja na Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwenda kuangalia nguo hizo.

“Tuangalie namna sare zilivyonunuliwa, aliyepewa zabuni alipatikanaje, sare zililetwa kutoka wapi? zikoje na kiasi cha fedha zilizotumika, ndio CAG aendelee kukagua,” alisema.

“CAG hawezi kutoka kwenda stoo kuangalia sare. Kwa hiyo Lugola alilipotosha Bunge kwa kuapa kuwa atavua nguo kama sare hazipo.”

Hata hivyo, Dk Tulia alimkatiza Kaboyoka, akimueleza anavyozungumza ni kama kwamba na yeye ni mchangiaji.

“Wewe ni mwenyekiti ambaye umekasimiwa madaraka ili uje ujibu hoja za wabunge na humpi mtu mwingine hoja. Baada ya kuzungumza wewe maazimio uliyotuletea na Bunge litaazimia.”

“Sasa kama unatupeleka kwenye hoja nyingine na wewe ndiye uliyeleta taarifa hapa ndani mwenyekiti utakuwa unaliongoza Bunge sehemu siyo.”

Alisema kama anayo hoja na kwenye kamati hawajamaliza ni juu yake.

Mdee ataka kamati teule

Katika mjadala huo, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alitaka chombo hicho cha kutunga sheria kiunde kamati teule kuchunguza sakata hilo la hati za kusafiria.

Halima alisema taarifa ya kamati inaonyesha namna gani inatoa malalamiko katika hoja zinazohusu ufisadi.

Alisema Serikali wamekuwa wazito kufanya uchunguzi na kwamba hilo limethibitishwa wakati mwenyekiti wa PAC aliposema walinyimwa mkataba wa e- passport na ufisadi wa sare za polisi.

Alisema kwa kuwa Bunge lina mamlaka ya kuunda kamati teule pale ambapo kuna utata na kwa kuwa kamati imeonyesha kuna shida kubwa pale inapoomba taarifa, “sasa nifanye utaratibu wa kuleta hoja rasmi kimaandishi ili Bunge lako liunde kamati teule ili tuweze kufukunyua ufisadi unaofichwa fichwa naomba kutoa taarifa”.

Lakini Dk Tulia alisema wakati mwenyekiti akijibu hoja za wabunge atapaswa kuwaongoza na si kuanzisha hoja nyingine.

“Kilichotokea leo (juzi jioni) ni mwenyekiti anaanzisha hoja wakati wa kuhitimisha hoja yake. Si kazi yake kuja kutuanzishia hoja hapa bungeni. Wameshindwa kufanyia kazi katika kamati, anakuja hapa wakati wa kuhitimisha kana kwamba anashtaki. Si utaratibu wa kikanuni,” alisema.

Mzozo wa kikanuni

Wengine waliochangia hoja hiyo ni mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa ambaye alisema katika suala la sare, Lugola aliweka rehani hata ubunge wake.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alimkatiza akitaka ufafanuzi wa utaratibu kwa kuwa kanuni zinataka kila mbunge kuchangia kilichoko mezani lakini Msigwa anachangia taarifa ambayo haikuwa mezani.

“Tukiendelea kupanua (hoja) kila mtu anavyotaka, tutashindwa kupata mwongozo wa kazi nzuri iliyofanywa na kamati,” alisema.

“Kwa hiyo tunatakiwa kujielekeza katika mjadala na kupata yale ambayo kamati imeleta. Hatuwezi kujua kwa nini kamati haikuleta mambo hayo yote.”

Akielezea suala hilo, Dk Tulia alisema mambo aliyokuwa akisoma Msigwa yanatokana na ripoti ya CAG na si ripoti ya PAC.

Aliporuhusiwa kuendelea, Mchungaji Msigwa alisema anashangaa Serikali kushindwa kujibu hoja za CAG kuhusu sare za polisi.

“Nani aliagiza sare za polisi? Alilipwaje Sh16 bilioni? Haya mambo si madogo. Lugola alisema ataweka rehani ubunge wake. Mwenyekiti tuambie hivyo vyote CAG alivyovidai vimepatikana?” Alihoji.

“Rais alisema juzi (Lugola) amelipwa Sh10 bilioni, amelipwajelipwaje?... epassport (hati za kusafiri za kielektroniki kuna faida gani? Inaonekana yanaleta faida hii. Zabuni ilikuwaje? Tuliingia zabuni na nani? Analipwaje? Passport moja gharama yake ni nini?”

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Anatropia Theonest alisema hoja ya e-immigration imepelekwa bungeni mara nyingi.

“Mtambo ulionunuliwa haukuwa recognized (hakutambulika), kwamba ulinunuliwa kiasi gani, zabuni ilifanyika wapi, ulikuwa na gharama gani lakini haukuletwa bungeni,” alisema.

Alisema Lugola alitumbuliwa kwa kushindwa kuleta mkataba bungeni, lakini pia mkataba wa e-immigration haukuletwa bungeni.”

Chanzo: mwananchi.co.tz