Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHAMBUZI WA MALOTO: Kamala Harris anavyompima ubavu Trump

Trump X Kamala UCHAMBUZI WA MALOTO: Kamala Harris anavyompima ubavu Trump

Thu, 25 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Ilionekana ingekuwa rahisi kwa Hillary Clinton, kumshinda Donald Trump mwaka 2016, haikuwezekana. Sasa, Kamala Harris anakaribia kuvalishwa glovu, ili aingie ulingoni dhidi ya Trump. Swali ni je, ataweza?

Rais wa Marekani, Joe Biden, amesalitiwa na umri pamoja na uchovu wa mwili. Ametii sauti ya Democrats wenzake wengi, walioona asingetosha kushindana na Trump. Biden amevua glovu, kisha ameomba avalishwe Kamala, kuelekea Uchaguzi wa Rais Marekani, Novemba 5, mwaka huu.

Kamala, baada ya mapendekezo ya Biden, alisema: “Kama ambavyo wengi wenu mtakuwa mnajua, kabla sijawa Makamu wa Rais, nilikuwa Seneta. Kabla yake nilikuwa Mwanasheria Mkuu wa California. Na kabla ya yote hayo, nilitangulia kuwa mwendesha mashtaka mahakamani.

“Katika maeneo hayo yote, nilishughulika na wahalifu wa kila aina. Mahayawani wanaonyanyasa wanawake. Matapeli wanaowaibia wateja. Wadanganyifu ambao huvunja kanuni kwa masilahi yao. Sasa nisikilize ninaposema, naijua aina ya Donald Trump. Na katika hizi kampeni nitajivunia sana kuweka rekodi zangu dhidi ya zake.”

Trump, baada ya Biden kumpendekeza Kamala, alisema: “Itakuwa rahisi kumshinda Kamala Harris kuliko ambavyo ingekuwa kwa Joe Biden.” Republicans wengi, pia wanaamini Kamala ni mwepesi kuliko ambavyo ingekuwa dhidi ya Biden.

Democrats kwa imani yao, Trump ni mwepesi, hivyo ilihitajika Biden akae pembeni, kisha yeyote mwingine anatosha kumshinda Trump. Baadhi wanatilia shaka nguvu ya Kamala, wanataka chama, Democratic, kimfikirie Hillary. Uchaguzi wa Rais Marekani 2016, watu milioni 231 walikuwa na vigezo vya kupiga kura. Watu milioni 128 walipiga kura. Zaidi ya kura milioni 60.5, zilimchagua Hillary, wakati Trump alipigiwa kura na wananchi milioni 60. Hillary alimshinda Trump kwa kura 439,902.

Marekani, Rais hupatikana kwa ya Kura za Majimbo (Electoral College). Wajumbe 538 wa Electoral College hupiga kura. Anayepata kura nyingi ndiyo hutangazwa Rais. Kwa mantiki hiyo, watu 270 pekee wanatosha kumfanya mtu kuwa Rais. Hillary alishindwa kwenye Kura za Majimbo.

Nguvu hiyo ya Hillary ndiyo inayowafanya wengine wadhani anaweza kumshinda Trump, kwa uhakika. Wapo wanaodhani Hillary amekuwa kimya muda mrefu, hivyo hauziki kuliko Kamala ambaye yupo kwenye mzunguko wa siasa, halafu anashika nafasi nyeti; Makamu wa Rais.

Sauti muhimu

Kuna wanasiasa wawili wanasubiriwa kutoa msimamo wao kuhusu Kamala kuwa mgombea urais; ni Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama na aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Marekani, Nancy Pelosi. Inaaminika kama Obama na Pelosi watamuunga mkono, itakuwa rahisi kwake kufanikisha tiketi ya kuwa mgombea urais wa chama cha Democratic.

Obama, alijitokeza haraka kumpongeza Biden kwa uamuzi wake wa kukaa pembeni kwenye mbio za urais. Hata hivyo, amebaki kimya kuhusu anayemuunga mkono.

Wapo wanaoutafsiri ukimya wa Obama kama ishara ya kutomuunga mkono Kamala. Kuna wanaosema kwamba Obama anasubiri muda mwafaka ufike ndiyo amuunge mkono Kamala.

Pelosi, Spika wa Baraza la Wawakilishi kipindi cha urais wa Trump. Wakati wao, mgongano ulikuwa mkubwa. Mara kwa mara mihimili ya Serikali na Bunge (Baraza la Wawakilishi), ilikuwa na migongano. Trump, Kiongozi wa Serikali, Pelosi, bosi wa Baraza la Wawakilishi, hawakuiva chungu kimoja kabisa. Kwa jinsi msimamo wa Pelosi ulivyo, bila shaka atataka kuona Democrats wanakuwa na mgombea mwenye msuli wa kumshinda Trump. Pengine ukimya wake ndivyo anatafakari kama Kamala anatosha au kinyume chake na kama hatoshi, basi nani mwingine?

Kuhusu maoni ya wananchi hadi sasa, Trump anaongoza. Taasisi nyingi za kiutafiti, kuanzia YouGov hadi Reuters, CBS News, Ipsos na kadhalika, zimetoa matokeo yanayoonyesha kuwa Trump yupo mbele dhidi ya Kamala. Tena, Kamala na Biden, ni kama viwango vyao vya kukubalika vipo sawa. Hivyo, hajabadili chochote.

Mtandao wa Bendixen wenyewe umeonyesha Kamala anamzidi Trump kwa pointi moja. Matumaini ya Democrats ni kwamba kipindi cha kampeni kitabadili upepo, kwa maana wengi watamuunga mkono kadiri siku zitakavyosogea na atakavyoweza kujinadi.

Rekodi za Kamala

Januari 20, 2024 Kamala alipokula kiapo aliweka rekodi tatu kwa wakati mmoja, kwanza ni mwanamke wa kwanza kusimama kama mgombea mwenza na kushinda kiti cha urais.

Pili, ni mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa rais wa Marekani. Tatu, ameandika rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Afrika na Asia, kushika nafasi kubwa zaidi Marekani.

Kwa kifupi, Marekani haikuwa imewahi kuwa na mwanamke aliyepata kushika nafasi kubwa mpaka Kamala alipokula kiapo Januari 20, 2021.

Mapema mwaka 2019, usingedhani kama Kamala angesimama kama mgombea mwenza. Alijitokeza kuwania tiketi ya Democratic kuwa mgombea urais. Ghafla akaanza kumshambulia Biden kuwa ni mbaguzi wa rangi. Desemba 2019, akajitoa kwenye mbio za kuwania tiketi ya Democratic na kumuunga mkono Biden.

Kipindi ambacho Kamala alikuwa anamshambulia Biden, ilikuwa mshangao kwa kila aliyefahamu uhusiano wao. Kamala alikuwa rafiki kipenzi wa mtoto wa Biden, Beau, aliyefariki dunia mwaka 2015 kwa ugonjwa wa saratani. Ni Beau aliyemkutanisha Kamala na Biden.

Kamala katika kitabu chake: “The Truths We Hold; An American Journey” – “Ukweli Tunaoukumbatia; Safari ya Mmarekani”, anaeleza kwa undani jinsi Beau alivyokuwa rafiki yake mkubwa. Nyakati ngumu za majukumu. Beau akiwa Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Delaware na Kamala Mwanasheria Mkuu wa jimbo la California.

“Tulikuwa tukizungumza mara kwa mara. Hata mara nne kwa siku,” anaeleza Kamala kufafanua jinsi ambavyo Beau alipata kuwa mshauri wake mkuu katika nyakati ngumu za kukabili majukumu yake kama Mwanasheria Mkuu wa California.

Hiyo ndio ikawa sababu watu kushangazwa na kitendo cha Kamala kumbadilikia Biden, baba wa Beau na kumwita mbaguzi.

Chanzo: Mwananchi