Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tupige marufuku makipa wa kigeni

Camara X Matampi X Diarra Tupige marufuku makipa wa kigeni

Tue, 3 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni muda wa kufanya uamuzi mgumu. Ni muda wa kutanguliza Taifa letu mbele. Ni muda wa kuitazama Taifa Stars kwa jicho la pekee.

Mojawapo kati ya eneo muhimu kwenye mchezo wa soka ni golini. Ni sehemu inayoamua hatima ya timu kuliko nafasi nyingine yoyote uwanjani. Ni sehemu ambayo hata makocha bingwa wote duniani hawapendi kupachezea chezea.

Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ bado ni changa. Bado iko kwenye safari ya kujitafuta Afrika. Mafanikio makubwa ni kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika.

Kwa sasa tuna timu tatu tu ambazo zinakupa uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa. Azam, Simba na Yanga. Wachezaji wengi wa Taifa Stars wanaitwa kutoka hizi timu tatu siyo kwa bahati mbaya. Kwanza mara nyingi zote ziko chini ya makocha wa kigeni ambao kiimani wengi wanakuwa na ujuzi pengine kuliko hawa wa ndani.

Wachezaji wanapata uhakika wa kucheza mechi nyingi za kimataifa iwe ni za ushindani au kirafiki. Wachezaji wa timu hizo tatu wanajifunza mambo mengi ya dunia.

Hawana ushamba hata kidogo. Timu zinawasaidia kusafisha macho. Kuwaonyesha vitu vipya. Bahati mbaya kwa sasa Azam, Simba na Yanga zote zina makipa wa kigeni ambao ni chaguo la kwanza. Hakuna kipa hata mmoja mzawa mwenye uhakika wa kuanza kwenye hizo timu. Hii ni hasara kwa Taifa. Hapa Taifa Stars huwa inakwenda kuumia.

Ni kweli kwa ukubwa wa klabu zetu tunahitaji makipa kama Djigui Diarrra na Moussa Camara, lakini kwa Taifa Stars ni hasara. Kocha wetu wa Taifa Stars anapata ugumu wa kupata kipa wa kuanza kwenye timu ya Taifa kwa sasa. Wote waliopo hakuna mwenye uzoefu wa mechi za kimataifa.

Wawili kati ya makipa watatu walioitwa hakuna anayeanza kwenye klabu. Pengine ni muda wa kuleta kanuni ya kuzuia makipa wa kigeni kuja kwenye ligi yetu. Hii kanuni itaumiza klabu, lakini itaisaidia sana Taifa Stars.

Kuna haja ya kutafakari sana eneo hilo. Ligi yetu inaonekana bado haina uwezo mkubwa wa kututengenezea kipa wa Taifa Stars. Ni kweli klabu nyingine nyingi zina makipa wazawa na ni machaguo ya kwanza. Ni kweli, lakini hawana ubora wa kuchezea Taifa Stars.

Simba, Yanga na Azam kwa ubora wa mazoezi, mechi nyingi za kimataifa, kuwa na wataalamu wengi wa kigeni inasaidia sana kumjenga kipa. Huu ni uamuzi mgumu ambao utasaidia sana kututengenezea kipa mpya wa uhakika. Bila uwepo wa Diarra, Abuutwalib Mshery angekuwa kipa bora sana pale Yanga. Bila uwepo wa Camara, Ally Salim angekuwa chaguo la kwanza pale Simba.

Uwepo wa makipa wa kigeni unaifanya Taifa Stars kuita makipa wanaokaa benchi kwenye klabu. Kupanga ni kuchagua. Tuumize klabu kwa faida ya Taifa letu. Eneo la kipa ndilo lililobeba mwelekeo wa timu. Ni sehemu muhimu ambayo haipaswi kuchezewa. Ndiyo maana huwa haibadilishwi badilishwi kama nafasi nyingine.

Taifa la Misri hapo nyuma liliwahi kuweka kanuni ya kuzuia makipa wa kigeni kucheza kwenye ligi na ilisaidia sana. Kupanga ni kuchagua, tufanye uamuzi. Nimeona kikosi cha Taifa Stars kikiwa na makipa wakaa benchi. Makipa chaguo la pili na tatu kwenye klabu zao. Walau mmoja kutoka Pamba  hupata nafasi.

Sio kwa ubaya, lakini natamani kaimu kocha Hemed Morocco angemuongeza na Aishi Manula. Pamoja na majeraha aliyopitia kwa muda mrefu. Pamoja na kukosa mechi nyingi za ushindani hivi karibuni. Bado  Manula ni kipa bora wa Taifa. Hatuna kipa yeyote kwa sasa anayekaribia hata nusu ya ubora wake. Nashauri kocha wa Taifa Stars amuongeze kwenye kikosi.

Nimeona amerejea kwenye Klabu ya Simba na tayari ameanza kucheza kwenye mechi za kirafiki. Manula ni Tanzania Wani kwa sasa. Ubora na uzoefu wake kimataifa ni faida kwa Stars. Tunataka kufuzu fainali za Afcon kwa kutumia makipa wa benchi? Makipa wasio na uzoefu kimataifa? Huko ni sawa na kubeti.Kama Taifa ni lazima tulitazame hili na kufanya uamuzi.

Kanuni ya kuzuia makipa wa kigeni kuna namna italisaidia Taifa. Tutapata vijana wengi wazawa watakaopewa nafasi kwenye klabu za Simba, Yanga na Azam FC. Kwa sasa hizo ndizo klabu zinazokupa uhakika wa kupata mechi nyingi za kimataifa kumudu presha na kushidnana kila siku kutafuta mataji.

Kitendo cha timu ya Taifa kwenda kucheza na kipa wa kubeti inatuumiza. Siyo kwa kudharau makipa walioitwa, ukweli ni kwamba bado Manula ni muhimu. Kocha aangalie namna ya kumuongeza kundini. Hata asipoanza, atasaidia kuzungumza na makipa wenzie kwa sababu ndiye mzoefu zaidi wa mechi za kimataifa kwa sasa nchini kuliko kipa mwingine yeyote.

Tupige marufuku makipa wa kigeni? Hilo ndilo swali dume. Kama klabu zetu zingekuwa na uwiano sawa wa maandalizi na ushindani, bila shaka yoyote ingekuwa rahisi kupata makipa wengine. Kwa sababu makipa wa klabu nyingine ubora ni mdogo sana, ndiyo maana hata kocha wa Stars imebidi achukue wakaa benchi. Hii imekaaje kwa makipa wa wazawa wengine wanaocheza kwenye klabu zao. Maana yake wasiocheza ni bora kuliko wanaocheza? Ni jambo la kutafakari.

Kanuni ya kuzuia makipa wa kigeni nchini itatutengenezea makipa wengi wazawa wenye uwezo wa kushindana. Azam, Simba na Yanga zinatupa makipa karibu 10. Kupitia kanuni baada ya miaka mitano tutakuwa na wazawa wengi wenye ubora na uzoefu wa mechi za Kimataifa.

Mashabiki wa Simba na Yanga wapunguze ubinafsi. Walitazame Taifa kwanza baadaye klabu. Najua kuna namna kanuni hiyo inaumiza klabu lakini ni kwa manufaa ya Taifa. Uzuri wa mpira ni mchezo wa maoni. Ni mchezo wa wazi kwa kila mtu. Inasikitisha sana kuona Taifa Stars haina uhakika na lango lake.

Kushinda ugenini dhidi ya Zambia kusitupe kiburi kuwa tuko salama. Tunahitaji kutengeneza uhakika wa muda mrefu na kwa kuanzia ni kuweka kanuni ya kuzuia makipa wa kigeni walau kwa miaka mitano ili tuone matokeo. Wenzetu wamewahi kufanya na imesaidia.

Tulinufaika sana na Manula kwa sababu amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Simba kwa miaka mingi. Naona sasa ameletewa washindani wa kigeni. Akipoteza nafasi, kama Taifa tutakuwa tumekwisha. Ndiyo nguo yetu pekee. Nashauri kaimu kocha wa Stars, Morocco amuongeze kikosini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: