Shirika la Umeme nchini (TANESCO) lipo katika hatua za mwisho kuandaa malipo ya fidia kwa wakazi wa wilaya zote zilizopitiwa na miradi ya ujenzi wa vituo 2 vya kupozea umeme katika wilaya za Sikonge na Urambo Mkoani Tabora.
Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Nishati January Makamba alipokuwa akiongea na wakazi wa kata ya Ipole wilayani Sikonge katika siku ya mwisho ya ziara yake Mkoani hapa.
Alisema fedha za malipo ya fidia ya Sh Bil. 1.6 kwa wananchi wote wapatao 746 ambao maeneo yao yalipitiwa na mradi huo zipo tayari baada ya kukamilika kwa zoezi la tathmini ya mazao na mali nyinginezo.
Alibainisha kuwa kwa sasa kinachosubiriwa ni Kamati ya Tathmini kupeleka orodha ya wafidiwa ili taratibu za malipo zianze huku Ofisa Mazingira wa Shirika hilo kutoka Makao Makuu Dkt Richard Myungi akiwahakikishia kuwa zoezi la ulipaji linatarajiwa kuanza mwezi ujao na kuhitimishwa mwezi wa tisa.
Awali, diwani wa kata Ipole John Mbogo na Mkuu wa Wilaya hiyo John Palingo walimwomba Waziri kuharakisha ujenzi wa kituo cha kupozea umeme Ipole ili kumaliza adha ya umeme katika wilaya hiyo.
Aidha walipongeza juhudi za serikali ya awamu ya 6 kwa kuwezesha vijiji 60 kati ya 71 vilivyoko katika wilaya hiyo kupata huduma ya umeme wa REA na kuomba vijiji 11 vilivyobakia navyo viunganishiwe huduma hiyo ikiwemo vitongiji vyote.
Walibainisha kuwa kati ya vitongoji 287 vilivyoko wilayani humo ni vitongoji 99 tu vilivyopata umeme huo, hivyo wakaomba serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kupeleka huduma hiyo katika vitongoji 188 vilivyobakia.
Waziri Makamba aliwahakikishia kuwa mradi wa Ipole (Sikonge) unaopeleka umeme hadi Katavi na ule wa Uhuru (Urambo) unaopeleka umeme hadi Kigoma itakamilika ndani ya mwaka huu wa fedha ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Alifafanua kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM imebainisha wazi kuwa huduma ya umeme itafikishwa katika vijiji vyote ikiwemo vitongoji, alibainisha kuwa zoezi la kupeleka umeme katika vijiji vyote linakamilika mwakani, baada ya hapo zoezi la kupeleka huduma hiyo katika vitongoji vyote litaanza.