Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sugu: Lowassa aliiongezea hadhi Chadema

SUGUUU WEB Sugu: Lowassa aliiongezea hadhi Chadema

Wed, 14 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) ameeleza namna Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa alivyokiongezea hadhi ya Chama cha Demokrasia Maendeleo (Chadema) mwaka 2015.

Akizungumza, Februari 13,2024 kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa kiongozi huyo aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita, Sugu amesema ujio wa Lowassa Chadema uliongeza hadhi ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Lowassa alihamia Chadema kutoka CCM baada ya kuwa miongoni mwa wagombea waliokatwa kwenye chama hicho wakati wa kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.

Baada ya Lowassa kuhamia Chadema na kuwa mgombea urais wa chama hicho, iliibuka sintofahamu hadi katibu mkuu wa wakati huo, Dk Wilbord Silaa kuamua kuondoka.

“Kiutendaji, alipojiunga na Chadema hakubadilisha chochote, kwani tulikuwa na mifumo kama taasisi, hata mwenyewe alisema nimeshangaa kukuta mifumo madhubuti kuliko alivyokuwa akisikia huko nje.

“Alipojiunga Chadema wakati ule, kuna vitu alituongezea, kikubwa alituongezea status (hadhi) kwa kuwa na Waziri Mkuu mstaafu kwenye chama.

“Pili alikuwa prominent figure (mtu mashuhuri), japo alijua hataweza kutangazwa hata akishinda, lakini alithubutu,” amesema.

Akizungumzia harakati za kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, Chadema ilipomsimamisha Lowassa kuwa mgombea wake wa urais, Sugu amesema kwenye mikutano yake yote kulikuwa na mafuriko ya watu na hiyo ni miongoni mwa alama nyingine.

“Tuliona kule Mwanza, Mbeya, alikuwa ni kiongozi anayekubalika. Tukiwa Mbeya kwenye kampeni, mara zote alinitia moyo kabla na baada ya mikutano, ni kiongozi ambaye Chadema ameacha alama nyingi.

“Kingine alichotuachia ni uwezo wake wa kuunganisha watu, alipokuja Chadema alituunganisha na watu, wengine kutoka CCM, tuliona nyomi (wingi) ya watu hadi kuitwa ‘mafuriko’ kwenye mikutano yetu,” amesem Sugu na kuongeza;

“Kingine cha kumkumbuka ni uvumilivu, hakuna mwanasiasa aliyesemwa sana kama Lowassa, mara ma-Richmond, lakini hutukusikia akitumia mamlaka yake kuamuru fulani akamatwe.

“Nakumbuka mara ya kwanza nakutana naye ana kwa ana ilikuwa bungeni nilipochaguliwa kuwa mbunge wa Mbeya Mjini, yeye akiwa mbunge wa Monduli, alinipongeza, akaniambia umeingia bungeni mwanangu.

“Mara nyingi nilikuwa nikikutana naye Dodoma, alipenda kuuliza hali ya chakula ilivyo Mbeya na misimu ya mvua, alipenda kuiongelea nchi zaidi,” amesema.

Sugu amema pia Lowassa alikuwa kiongozi mwenye mawazo yenye uthubutu, japo baadhi ya watu binafsi walimkwamisha kufikia malengo.

“Amekuwa mpambanaji kwenye uongozi, katika siasa za Tanzania alikuwepo muda mrefu hadi kuwa waziri mkuu, tulikuwa tunaona alivyopambania nchi, ikitokea kiwanja fulani tajiri mmoja anataka anunue, yeye alizuia.

“Kuna nyakati tulimuona yuko Singida anasaidia kusukuma gari lililokwama kwenye tope, sifa zile ndizo zimemuweka karibu na wananchi,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live