Utamu wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo kwa michezo miwili, huku macho ya mashabiki yakiwa kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida wakati wenyeji Singida Black Stars watakapovaana na KMC, huku kocha Patrick Aussems akitamba kutaka kuendeleza ubabe ili kuvuna pointi zaidi katika ligi hiyo.
Singida ilianza msimu kwa kishindo kwa kupata ushindi wa mechi mbili mfululizo ikiwa ugenini, ikianza kwa kuwachapa wageni wa ligi hiyo, KenGold jijini Mbeya kwa mabao 3-1 kisha kuichapa Kagera Sugar kwa bao 1-0 mjini Bukoba na leo itacheza kwa mara ya kwanza nyumbani kwa msimu huu dhidi ya KMC.
Ni mechi inayozikutanisha timu zinazofundishwa na makocha wa kigeni, huku zikiwa hazichekani katika mechi sita walizokutana katika ligi hiyo tangu mwaka 2020 wakati Singida ikifahamika kama Ihefu.
Katika mechi hizo sita zilizopita timu hizo kila moja imeshinda mechi tatu, huku kukiwa hakuna sare yoyote baina yao na kila timu imefunga mabao manne na kufungwa manne, japo msimu uliopita katika mechi ya Kombe la Shirikisho, KMC ilicharazwa nyumbani kwa mabao 3-0 na Singida BS ikitumia jina la Ihefu.
Kutokana na hali hiyo ni wazi pambano la leo likipigwa saa 10:00 jioni linatolewa macho na kila upande ili kujiongezea heshima ndani ya msimu huu, huku Singida ikitaka ushindi ikae kileleni kuing'oa Simba wakati KMC ikisaka ushindi wa kwanza kwani mchezo wa kwanza dhidi ya Coastal Union ilitoka sare ya 1-1.
Akizungumza na Mwananchi, Aussems alisema hawataki kufanya makosa kwenye uwanja wao wa nyumbani watautumia vyema kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kuendelea kusonga mbele kwa kuhakikisha wanafikia malengo yao ya msimu.
"Hautakuwa mchezo rahisi tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wetu tukiwa na lengo moja la kupambania matokeo mazuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani matokeo yaliyopita hayawezi kuwa sababu ya sisi kujiamini tumekiandaa kikosi tayari kwa ushindani." Alisema.
Kocha wa KMC, Abdulhamid Moalin alisema amekiandaa kikosi chake vizuri tayari kwa ajili ya kusaka pointi tatu muhimu kuelekea mchezo wao wa leo ugenini.
"Hatukuwa na matokeo mazuri kwenye mchezo wetu wa mwisho wa ligi kabla ya ligi kusimama kupisha mechi za timu za taifa tukiambulia sare dhidi ya Coastal Union nimefanyia kazi makosa naamini tutakuwa na mchezo mzuri mbele ya Singida Black Stars," alisema Moalin.
Timu zote zitategemea nyota wao hatari, KMC ikimtegemea zaidi Ibrahim Elias, Daruwesh Saliboko, Kenny Ally, Rashid Chambo na Juma Shemvuni, huku Singida ikiwa na majembe ya maana kama Elvis Rupia, Habib Kyombo, Emmanuel Keyekeh, huku ikiwa na nafasi finyu ya kuwapa nyota waliokuwa timu za taifa kama Marouf Tchakei, Mohammed Camara.