Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewataka Wahitimu wa Mafunzo ya awali ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwenda kuzuia na kupambana na tatizo la rushwa kwenye miradi mikubwa ya kijamii inayoendelea kutekelezwa sehemu mbalimbali nchini kwani Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Waziri Simbachawene amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora zaidi kwa kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ikiwemo elimu, afya pamoja na maji inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sio kuingia katika mifuko ya watu wachache.
Simbachawene ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya kufunga Mafunzo ya awali kwa Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi 370 wa TAKUKURU yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro. - Waziri Simbachawene amesema, maono na malengo ya Serikali ni kuhakikisha wahitimu hao wanakwenda kuzuia rushwa na ikishindikana kuzuia wakapambane nayo kwani rushwa inapofusha na ni ukosefu wa ustaarabu katika jamii.
Katika hatua nyingine Simbachawene ametoa rai kwa wahitimu hao wa TAKUKURU kutulia katika vituo vya kazi watavyopangiwa na kuachana na mawazo ya kuhamia sehemu nyingine kwa madai ya kutafuta masilahi zaidi.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni amesema ajira hizo kwa wahitimu hao zilikuwa ni za kimkakati lengo likiwa ni kuhakikisha maeneo yaliyokuwa hayawezi kufikiwa na TAKUKURU yanafikiwa kwa sasa na kwa urahisi zaidi.
ββMhe. Waziri hawa wahitimu unawaona wengi wao ni Maafisa ambao ni wahitimu katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini katika maeneo tofauti wakiwemo Mainjinia lengo letu ni kuhakikisha mianya yote ya rushwa inadhibitiwa, CP Hamduni ameongeza.ββ