Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simbachawene atoa masharti makanisa

E9ae3d2ebe940af429e3600df1dfc043.jpeg George Simbachawene, Waziri wa Mambo ya Ndani

Mon, 20 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewataka mitume na manabii kuhakikisha wanamaliza tofauti zao kabla ya kuomba usajili wa makanisa yao. Simbachawene aliyasema hayo alipohudhuria Kongamano la Mitume na Manabii lililofanyika Dar es Salaam.

“Sheria ya Uhuru wa kuabudu Ibara ya 19 imeweka bayana mahusiano ya serikali na utatuzi wa migogoro ya viongozi wa dini au nyumba za ibada, mara nyingi serikali inachelewesha usajili wa taasisi zenu kutokana na kuwa na migogoro baina yenu, Mmeanza vizuri mkajenga hekalu lakini ikatokea kutoelewana mmoja anang’oa bati, mwingine anachukuwa kinanda wakati suala la usajili linaendelea..., laa hasha, inapotoekea hali kama hiyo tunasitisha kwanza kwa sababu haturuhusiwi kisheria kuwaingilia isipokuwa inapotokea viashiria vya uvunjifu wa amani ndipo tunapoingilia,”alisema.

Simbachawene alitoa kauli hiyo kutokana na swali lililoulizwa na Ado November ambaye pia ni mwimbaji wa Nyimbo za Injili aliyetaka kujua kwa nini kuna urasimu wa usajili wa makanisa nchini.

Simbachawene aliwaeleza mitume na manabii kuwa sheria ya usajili wa jumuiya mbalimbali nchini hususani Kanisa sharti liwe taasisi, siyo mali ya mtu na liwe na watu kuanzia wawili na uendelea lakini siyo mtu peke yake anaenda kusajili Kanisa jambo lisilokubalika na ndio chanzo cha usajili kuchelewa.

Akizungumzia kufutwa kwa msamaha wa kodi kwa taasisi za kidini, Simbachawene alisema makosa ya kiufundi yanafanywa na baadhi ya viongozi wenyewe wa dini kwa kutoa taarifa danganyifu.

“Kiongozi wa Kanisa anaomba msamaha wa kodi, anaagiza gari kwa matumizi ya uinjilishaji au useminari, kesho gari hiyo inafanya shughuli za uwindaji au za kitalii, basi aisajili kibiashara ili alipe kodi...baada yakuyagundua haya madudu ndipo tukawa wakali, tunataka tuone matokeo ya dhumuni la msamaha wa kodi husika,”alisema.

Kuhusu tuhuma za baadhi ya makanisa kuwapigia kelele na kubughudhi wengine, alisema kelele ni moja ya kero zilizoainishwa kwenye sheria ya mazingira na kusema kuwa vivyohivyo viongozi wa dini wanapotaka kuheshimiwa wanapaswa pia kuheshimu uhuru wa wengine . Aliwataka watafute maeneo ambayo ni makubwa na sala, kusifu na kuabudu kufanyike kwa taratibu maalumu siyo kila dakika na kila saa.

“Binafsi kero hiyo nishakumbana nayo, jirani yangu na rafiki yangu kaanzisha Kanisa, Mzee wangu yaani Baba alikuwa na shinikizo la damu nikamuendea ikawa Ijumaa usiku wana mkesha hadi asubuhi kufika saa 5:00 usiku hali ya Baba imebadilka nikamwendeana walipunguza sauti, Kunahitajika utaratibu unaofaa lakini pia kuwe na kiasi kama sauti ya kawaida haifai kufikisha ujumbe mbona hapa tunaelewana, yaani umeshindwa kumvuta jirani yako aje kusali kwako unapiga sauti ya juu ili wa mbali waje? kama umeshindwa kumpata wa karibu wa mbali utampataje?” alihoji.

Hata hivyo Simbachawene aliwataka Manabii na Mitume kuwa waadilifu na waaminifu ili kupata wataalamu waaminifu serikalini. “Kiongozi wa dini ukiwa tapeli utatuletea mbunge tapeli, waziri tapeli, Mkurugenzi tapeli,sisi sote tunatokea katika taasisi za dini, onesheni mfano,”alisema.

Viongozi hao walimshukuru Simbachawene kuhudhuria Kongamano hilo na kuahidi kuipa serikali ushirikiano wa kutosha katika kuendesha nchi hususani kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake ili amani na maendeleo ya nchi yapatikane.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live