Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewataka maofisa rasilimali watu na maofisa sheria kutoka katika sekretarieti za mikoa na halmashauri za wilaya kutumia weledi katika kutoa ushauri wenye tija kwa maofisa masuuli ili kuepuka hasara serikalini.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo mkoani Dodoma wakati wa kikao kazi cha maofisa rasilimali watu na maofisa sheria ambapo amewataka maofisa hao kuzingatia sheria na kanuni za usimamizi wa rasilimali watu katika utumishi wa umma.
Amebainisha kuwa taasisi za umma zinapokuwa na malalamiko mengi ya watumishi ni ishara kuwa watendaji wa ofisi hizo hawafanyi kazi ipasavyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi, Juma Mkomi amesema maofisa hao ni washauri wakuu wa maofisa masuuli katika taasisi zao, hivyo wanatakiwa kutoa ushauri kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka kuwaumiza watumishi.