Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameutaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuweka nguvu zaidi katika kuziingiza kaya maskini zenye watu wenye ulemavu kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ili nao waweze kujiinua kiuchumi na kufikia malengo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatamani kuona mpango huo unagusa makundi mengi zaidi yenye uhitaji.
Simbachawene ameyasema hayo leo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji cha Kinywang’anga Wilaya ya Iringa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF.
Amesema TASAF imekuwa mkombozi kwa wananchi wanaonufaika kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na mpango huo huku akisisitiza kuwa katika awamu ijayo iwaangalie zaidi watu wenye ulemavu kwani wamekuwa wakikosa fursa nyingi kulingana na changamoto walizokuwa nazo.
"Kaya zenye watu wenye ulemavu na hazijiwezi kimaisha zina mzigo mara mbili ukilinganisha na kaya zisizojiweza na hazina watu wenye ulemavu, hivyo ni lazima kaya zenye walemavu zipewe kipaumbele zaidi" amesisitiza Mhe.Simbachawene
Amesema moja ya dhamira Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kaya maskini zenye walemavu zinapata uhakika wa milo mitatu kama zilivyo kaya nyingine masikini.
Hata hivyo Simbachawene amesema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha fedha zinazotoka zinafika kila mahali na kwa walengwa sahihi hasa waishio vijijini katika kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya TASAF.
Amesema miradi inayotekelezwa na TASAF inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja na kushirikisha jamii katika uhalisia wake akisema huo ndio msingi wa viongozi wa Tanzania.
“Lengo la miradi la TASAF ni kuondoa umasikini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja na kaya, ndio maana kuna wanufaika wanaopewa fedha za moja kwa moja ili kuwapa ahueni katika hali zao za maisha,” amesema Simbachawene.