Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simbachawene ataka wanasiasa kuheshimu kazi za kitaalamu

Chawenepic George Simbachawene, Waziri wa Mambo ya Ndani

Thu, 21 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewataka wanasiasa kutoingilia kazi za wataalamu na kukosoa ikiwa hawana ujuzi kwa wanachokosoa.

Simbachawene amesema hali hiyo inawakatisha tamaa na kuwavunja mioyo baadhi ya wakandarasi hasa wazawa hivyo akataka uwe unafanyika uchunguzi kwanza kabla ya kukosoa.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 21, 2021 Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa 10 wa Chama cha Wakandarasi Wazawa (ACCT).

Waziri amesema kitendo cha kukosoa bila kuwa na utaalamu kwa unachokosoa kinapaswa kuangaliwa ili kutokuingilia mambo ya kitaalamu zaidi.

Kauli ya Simbachawene imekuja katika kipindi ambacho kimekuwa na wimbi la kukataliwa kwa miradi mingi ya Serikali kwamba imejengwa chini ya kiwango.

"Nadhani wanasiasa tuheshimu kazi za kitaalamu, unawezaje kukosoa kitu ambacho huna ujuzi nacho, ufike wakati tutazame hili na kama inabidi basi tupate ushauri kwa wataalam kwanza," amesema Simbachawene.

Hata hivyo amewaomba wataalam kwa upande wao kuheshimu kauli za watunga sera na viongozi wa kisiasa ili wasiingiliane katika majukumu.

Amesema makundi hayo yakiheshimiana inaweza kusaidia kazi za Serikali kujengwa kwa kiwango na inapobidi ukaguzi wake ufanywe na watu wenye utaalamu kwenye maeneo hayo.

Kuhusu wakandarasi wazawa amewataka kubadilika katika kazi zao kwa kuongeza ubunifu na kujenga kwa ubora lakini katika muda unaokubarika ili waendelee kuaminika.

Chanzo: mwananchidigital