WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene jana amefanya ziara katika eneo la Mradi wa Ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Uhamiaji, Jijini Dodoma na kutoa maelekezo kwa Kampuni ya Ujenzi ya SUMAJKT kufanya kazi Saa 24.
Simbachawene amemtaka Mkandarasi wa Mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili jengo hilo liweze kukamilika kwa haraka.
Amesema jengo hilo la ghorofa nane lilipaswa kukamilika mwezi Desemba, 2020, lakini mpaka sasa lipo asilimia 41 jambo ambalo hajaridhishwa nalo.
Hata hivyo Simbachawene alitoa pongezi kwa Mkandarasi huyo kwa kujenga jengo lenye ubora mkubwa litakalochangia katika kuboresha huduma bora za Ki-Uhamiaji zinazokidhi viwango vya Kitaifa na Kimataifa.
"Jengo hili litakapokamilika linaweza kuwa la kwanza hapa Dodoma kwa ukubwa, hivyo nawataka wajenzi hawa kuongeza kasi ili tuweze kuhamia hapa mapema iwezekanavyo," alisema Simbachawene.
Idara ya Uhamiaji inaendelea kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwemo kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu kupitia utekelezaji wa sheria na kanuni zilizopo ili kulinda usalama wa Taifa na kukuza maendeleo ya Kichumi huku ikiongozwa na Kauli mbiu ya Uhamiaji, “Usalama na Maendeleo”