Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simbachawene aonya askari wanaosaidia wahamiaji

26b9dcf4f36448d682a4fe63469b26c9 Simbachawene aonya askari wanaosaidia wahamiaji

Mon, 18 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imesema itawawajibisha ikiwamo kuwachukulia hatua kali askari watakaobainika kuwasaidia wahamiaji haramu wanaopita nchini kwenda nchini nyingine.

Onyo hilo lilitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene wakati akifungua mafunzo ya uhamiaji na uongozi katika kambi ya Boma Kichakamiba wilayani Mkinga, mkoani Tanga juzi.

Alisema Tanzania imekuwa ikitumika kama njia ya wahamiaji hao kupita kwa urahisi kwenda katika nchi wanazotaka, hivyo serikali itaanza kuchukua hatua kwa askari watakaobainika kutumika kuwasaidia kwa namna moja au nyingine.

"Wahamiaji hao wameona njia salama ni baharini, niutake mkoa wa Tanga usiwe njia ya kupitisha wahamiaji haramu na endapo watapita na kukamatwa katika mkoa mwingine, Jeshi la Polisi na Uhamiaji watawajibika," alisema.

Aidha, Simbachawene alisema hatasita kuwafuta kazi watumishi watakaojihusisha na vitendo hivyo.

Hata hivyo, alisema mafunzo kwa maofisa hao ni muhimu kwa sababu yatasaidia kuwaongezea mbinu za kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu na wizara hiyo itaendelea kutoa ushirikiano.

Akitoa taarifa ya chuo hicho, Kamishna wa Uhamiaji nchini, Dk Anna Makakala alisema kambi ya Boma Kichakamiba ina wanafunzi 287, wanawake 81 na wanaume ni 206.

Alisema lengo la kuanzisha kambi hiyo ni kukidhi mahitaji ya idara kuwa na askari wenye weledi na ari ya kufanya kazi kwa ufanisi ili kufikia malengo ya serikali.

"Ili kupata askari wenye weledi, nidhamu na maadili ya kazi ya uhamiaji sasa askari hao watapata mafunzo katika chuo chao badala ya hapo awali walikuwa wakipata mafunzo katika vyuo tofauti," alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela aliwataka wananchi wa Mkinga kutoa ushirikiano kwenye kambi hiyo huku akiwataka kuchangamkia fursa ya kiuchumi kwa kuweka huduma za kuuza chakula katika maeneo yao.

"Niwaombe wananchi msivamie maeneo yaliyotengwa ya chuo hiki kwa kigezo kuwa hayajaendekezwa, hivi vichaka vilivyopo ndio sehemu ya utendaji kazi wa majeshi yetu, hivyo wapeni ushirikiano ili waweze kutimiza lengo la uwanzishwaji wa kambi hii," alisema Shigela.

Chanzo: habarileo.co.tz