MGOMBEA ubunge Jimbo la Kibakwe katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), George Simbachawene, amesema akichaguliwa, ataimarisha miundombinu ya barabara ya lami kutoka Njia Panda Kongwa hadi Chipogolo ili kuikuza miji ya Mpwapwa na Kibakwe.
Simbachawene, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, aliyasema hayo katika uzinduzi wa kampeni jimboni Kibakwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu kuchagua rais, wabunge na madiwani.
Kabla ya kueleza vipaumbele vyake, alitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020.
Alisema, akichaguliwa atahakikisha Kibakwe inafunguka kimaendeleo kwa kufungua barabara ya Chipogolo Rudi hadi Kibakwe kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa za biashara na uchumi katika jimbo hilo.
Alitaja vipaumbele vyake vinne alivyodai ataanza navyo akiingia madarakani kuwa ni kuimarisha miundombinu, ubora wa huduma za elimu, maji na huduma za afya.
"Nitahakikisha naanza na miundombinu yaani barabara, elimu, maji na afya, nataka kuifanya Kibakwe iwe mpya," alisema Simbachawene.
Naye mgombea ubunge Jimbo la Dodoma Mjini, Antony Mavunde, alisema aliwataka Wanakibakwe kutambua na kuthamini mchango wa Rais John Magufuli katika maendeleo yao na jimbo kwa jumla, hivyo wampe shukrani zao kwa kumpigia kura siku ya uchaguzi ikiwadia.
"Ifikapo Oktoba 28, lazima tupige kura za shukrani kwa Rais Magufuli na Simbachawene ili wapinzani wasirudie kuchukua fomu," alisema Mavunde.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mpwapwa, George Chigwie alisema kitendo cha baadhi ya waliokuwa wapinzani wa Simbachawene katika kura za maoni kwenda kwenye mkutano huo kinaonesha umoja na ushirikiano kati wagombea wa chama hicho.
"Kitendo cha washindani wake waliokuwapo kwenye kura za maoni kuja kumuunga mkono, kinatupatia matumaini makubwa kuelekea siku ya uchaguzi, Oktoba 28, 2020," alisema Chigwie.