Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameiagiza Taasisi ya Watumishi Housing Investments (WHI) kuja na ubunifu wa kujenga makazi bora ya watumishi wa umma katika maeneo ya mijini yaliyo jirani na maeneo ya shule na hospitali.
Amesema kama nyumba hizo zitajengwa maeneo jirani na wanakofanyia kazi zitawaondolea changamoto zinazojitokeza na kupunguza ufanisi wa kazi.
Amesema maeneo ya mijini, shule na hospitali zinamiliki maeneo makubwa ambayo taasisi ya WHI inaweza kuyatumia kujenga majengo marefu kwenda juu ili kuwafanya walimu na manesi wafurahie kutoa huduma kwa wananchi kwa kuishi kwenye makazi bora jirani na maeneo ya kazi.
Simbachawene ametoa kauli hiyo leo, Januari 9 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na timu ya Menejimenti ya Taasisi ya Watumishi Housing Investments (WHI) ikiwa ni muendelezo wa kusikiliza changamoto zinazoikabili taasisi anazozisimamia na kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa wakati wa ziara aliyoifanya Agosti mwaka jana.
''Hakuna asiyejua umuhimu wa walimu na manesi katika nchi hii lakini lakini wengi wao wamekuwa wakiishi maeneo ya mbali na wanakofanyia kazi na hivyo kulazimika kulipa nauli kubwa kwa vile hawawezi kumudu kulipa kodi ya makazi yaliyo jirani na maeneo yao ya kazi, waguseni hawa kwa kuwajengea makazi bora,” amesema Simbachawene.
Mkurugezi wa Taasisi ya Watumishi Housing, Dk Fred Msemwa amesema kwa mwaka 2023/ 24 wameendelea na ujenzi wa nyumba Njedengwa, Magomeni na Gezaulole lengo likiwa ni kupunguza adha wanazozipata watumishi wa umma wakiwemo walimu na manesi.