WAZIRI wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, amesema atafagia kwa kuwaondoa kazini askari wote watakaoshindwa kudhibiti wahamiaji haramu maeneo ya mipakani
Simbachawene ameyasema hayo mkoani Tanga na kwamba atashugulikia askari wote watakaozembea wahamiaji kuingia kwa njia za panya kwenye mikoa iliyo mipakani.
Simbachawene amesema kitendo cha wahamiaji haramu kukamatwa maeneo mbalimbali ndani ya nchi, ambayo siyo mipakani ni kutokana na kuwepo mawakala wanaofanikisha wahamiaji hao kuingia nchini.
“Wahamiaji haramu kama tukiwakamata Morogoro na wakasema wameingia hapa Mkinga, sisi hatushughuliki na wale Morogoro, tutashughulika na waliopo wilayani Mkinga na Tanga, tuwahoji wamepitajepitaje wahamiaji hawa haramu hadi kuingia nchini,” amesema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “Pia tutawauliza polisi, ilikuaje msiwaone wahamiaji hawa haramu maana ‘barrier’ zote zenu, hawa hawatembei kwa miguu, walipanda gari, walipandia wapi gari? wakituambia walipanda gari, hawa watu wote (Askari Polisi na Uhamiaji) wapo kwenye Wizara yangu, wote nitafagia.”