Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, George Simbachawene amewasihi Wanafunzi kusoma kwa bidii na kuacha kujidanganya kuwa elimu kwa sasa haina umuhimu kwa kuwa hata waliosoma wamekosa ajira na wapo Mtaani.
Simbachawene ametoa nasaha hizo wakati wa mahafali ya 19 kwa Wanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Rudi iliyopo katika Kata ya Rudi, Wilaya ya Mpwapwa Mkoami Dodoma.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dkt. Samia Suluhu Hassan amelenga kuboresha elimu na kuifanya elimu ya kidato cha nne kuwa ya lazima na sio hiyari na hivyo, Wananchi wa Jimbo la Kibakwe wananufaika pia na maono hayo.
“Ninawaomba Wananchi wote wa Jimbo la Kibakwe kupitia kwenu ninyi wazazi wa watoto hawa wanaofanya mahafali yao leo, kutambua kuwa mtu aliyemaliza kidato cha nne ana uwezo mkubwa wa kuchambua mambo kisayansi ukilinganisha na yule wa darasa la saba, hivyo elimu ni muhimu kwa kuwa inaongeza uwezo wa kufikiri na kupanua uelewa wa namna bora ya kupambana na changamoto.”