Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simanzi na vilio mwili wa Lowassa ukiagwa Monduli

Lowassaaa 55986400 Mwili wa Lowassa ukiagwa

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maelfu ya wananchi walijitokeza jana kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, nyumbani kwake kijijini Ngarash, Monduli mkoani Arusha.

Wakati wa tukio hilo, vilio na simanzi vilitawala kutoka kwa wanaume, wanawake na watoto walipopita mbele ya jeneza kutoa heshima zao za mwisho. Shughuli  za kuaga mwili wa Lowassa nyumbani hapo ziliongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

Akizungumza wakati wa ibada ya kutoa heshima za mwisho, Pinda aliwataka Watanzania kumkumbuka Lowassa kwa mambo mazuri aliyofanya katika nchi na taifa.

Alisema akiwa serikalini alifanya kazi vizuri na Lowassa na kuna mambo mengi aliyojifunza kutoka kwake.

"Hatua aliyofikia Edward Lowassa anahitaji kufanyiwa maombi ili Mwenyezi Mungu aweze kumfungulia milango ya mbinguni. Pia tujaribu kumkumbuka kwa mengi aliyofanya," alisema.

Pinda alisema Lowassa alikuwa anasimamia kile alichotaka kufanya katika utendaji kazi wake, hivyo alitoa rai kwa Watanzania kuiga mema aliyoyafanya na kuyaendeleza kama ishara ya kumkumbuka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, alisema Lowassa alikuwa mtu wa watu mwenye marafiki wengi na alifanya kazi iliyotukuka ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Kuna mambo aliyofanya ikiwemo kuacha alama kwa nchi yetu na Chama Cha Mapinduzi wakati akiwa mtendaji ndani ya serikali na chama,” alisema.

"Sisi kama viongozi wa serikali tumebeba jukumu la kusimamia na kuhitimisha hadi hapo tutakapompumzisha na kumhifadhi kwenye nyumba yake ya milele,” aliongeza.

Mhagama aliwaomba wananchi kujenga utamaduni wa kuwaombea viongozi katika utendaji kazi kwa kuwa wametwishwa jukumu la kuwahudumia.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wenyeviti wa CCM nchini, alisema Lowassa alikuwa mtu wa watu na kiongozi mahiri na makini.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Abel Mollel, alisema Lowassa alikuwa mshiriki mzuri na mwaminifu wa maendeleo ya kiroho kwenye madhehebu ya dini ya Kikristo na kwamba hata kwa dini nyingine alitoa michango yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Balozi Ephraim Mafuru, alisema kituo hicho kinamkumbuka Lowassa kwa kuwa alipokuwa mkurugenzi mtendaji, alileta mabadiliko makubwa ikiwamo mageuzi katika sekta ya utalii na uchumi wa kumbi za mikutano ili kuwavutia wageni wanapoingia nchini kutembelea vivutio vya utalii.

Mkuu wa Mkoa wa Singida mstaafu, Parseko Kone, akizungumza kwa niaba ya marafiki wa familia ya Lowassa, alisema kiongozi huyo alikuwa mchapakazi na mwenye upendo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live