Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheria Madini kufumuliwa kuruhusu biashara makinikia

Hamza Johari Fdgdf Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari

Tue, 3 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sheria ya Madini, Sura ya 123 imefumuliwa kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2024, na kuruhusu biashara ya makinikia ndani ya nchi ambayo awali ilikuwa imezuiliwa ili kuvutia uwekezaji katika viwanda vya madini ghafi nchini.

Akisoma maelezo ya muswada huo Bungeni jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, alisema sheria hiyo ilitungwa mwaka 2010 na hadi sasa imefanyiwa marekebisho mara 13.

Alisema marekebisho yanapendekeza kurekebisha jumla ya vifungu 12 na vifungu vipya viwili vinapendekezwa kuongezwa, ibara ya 21 ya Muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha IOOD, ili kuruhusu biashara ya makinikia ndani ya nchi. Kwa sasa sheria inazuia biashara ya makinikia ndani na nje ya nchi.

Aidha, alisema Ibara ya 22 ya Muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 106 ili kuwataka wafanyabiashara wa madini walio na leseni na mawakala au madalali walio na leseni kuapa kiapo cha uadilifu na inalenga kuhakikisha utii wa sheria. “Ibara ya 13 ya Muswada inapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 271 ili kuanzisha Maabara ya Madini ya Tume ya Madini. Lengo la marekebisho hayo ni kuirasimisha taasisi hiyo na kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa msingi wa sheria,” alisema.

Alisema Ibara ya 14 ya Muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 66 ili kuweka adhabu kwa mtu atakayeshindwa kulipa ada ya ukaguzi kama ilivyoainishwa katika sheria.

Pamoja na hayo, alisema ibara ya 15 ya Muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 73 ili kutofautisha leseni za wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite na wafanyabiashara wa madini ya vito vingine vya rangi.

“Lengo la marekebisho haya ni kuweka udhibiti wa madini ya Tanzanite kwa namna maalumu na kuyatangaza kwa kuzingatia uwapo wa madini hayo wa kipekee nchini Tanzania,” alisema.

Alisema Muswada unapendekeza marekebisho katika kifungu cha 86A ili kuweka masharti kwamba mwingizaji wa madini nchini hatatakiwa kulipa mirabaha kwa madini yanayoingizwa nchini endapo atathibitisha kuwa amelipa mirabaha katika nchi yalikotoka madini ili kuepusha ulipaji wa mirabaha zaidi ya mara moja.

“Muswada unapendekeza marekebisho katika kifungu cha 87 kwa kuongeza viwango vya mirabaha inayopaswa kulipwa serikalini na wafanyabiashara wa madini ya vito yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi ambayo yamenunuliwa katika minada ya madini na maonyesho ya kimataifa ya madini ya vito,” alisema.

Pia, alisema Muswada unapendekeza marekebisho katika kifungu cha 27 F ili kuweka adhabu kwa wamiliki wa haki za madini ambao wanatoa taarifa za uongo au zenye kupotosha au kushindwa kuwasilisha taarifa sahihi za madini.

Pia alisema Ibara ya 14 ya Muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 66 ili kuweka adhabu kwa mtu atakayeshindwa kulipa ada ya ukaguzi kama ilivyoainishwa katika sheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live