Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa ufafanuzi vituo bandia vya kujiandikisha

Mohamed Mchengerwa 1080x640 Serikali yatoa ufafanuzi vituo bandia vya kujiandikisha

Wed, 16 Oct 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amesema yapo maneno yanazungumzwa kuwa kuna vituo bandia vya kuandikisha wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa kitongoji kimoja kina kituo zaidi ya kimoja.

Akitolea ufafanuzi suala hilo Mchengerwa amebainisha kuwa jambo hilo lilikwishaelekezwa, hivyo warejee kwenye taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali ya Oktoba 10, 2024 siku moja kabla ya kuanza uandikishaji ambapo alifafanua kuwa uandikishaji huo unatarajiwa kufanyika katika vituo 80,812.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Mwanza Waziri Mchengerwa ametaka ifahamike kuwa kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba 796 na 797 kuhusu orodha ya maeneo yatakayoshiriki uchaguzi, inajumuisha jumla ya mitaa na vitongoji 68,543 na kwamba lengo la kuwa na vituo vidogo ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa ili kupata haki yao ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa.

Amesema hiyo ina maana kuwa vipo vitongoji na mitaa ambayo kuna kituo zaidi ya kimoja na hilo limekuwa likifanyika miaka yote ya uchaguzi kutokana na wingi wa watu na jiogarafia ya mahali ya eneo husika.

Amesisitiza kuwa kutowafikishia wananchi fursa hiyo ni kuwanyima haki yao ya kikatiba na kwamba pale inapobainika kuna uhitaji wa kituo cha kuandikisha na kupiga kura, kanuni zinaelekeza vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi katika eneo husika kukubaliana na kuamua ni wapi kituo kiwekwe ili kuhakikisha wananchama wao na wananchi wengine wote wanapata fursa hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live