Serikali imekanusha madai ya wanawake kunyanyaswa na mifugo kuchukuliwa na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi Tanzania (Tanapa) yaliyotajwa kufanyika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Kauli hiyo ni sehemu ya taarifa ya Serikali iliyotolewa bungeni jana Mei 15,2023 na Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa, alipokuwa akitoa majibu na nini kinaendelea wilayani huko baada ya mbunge wa Jimbo kulalamika.
Mbunge wa Mbarari (CCM), Francis Mtega aliomba kutoa hoja ili bunge liahirishwe shughuli zake Mei 11, 2023 na kujadili alichosema kilikuwa kimefanyika katika jimbo lake.
Kwenye hoja zake mbunge huyo alieleza namna ambayo Tanapa wameumiza wananchi, kuuwa mifugo lakini kufanya alichosema ni uporaji wa mifugo (200) ya mfugaji jambo lililopelekea mhusika kutaka kujinyonga.
Kauli hiyo ilimfanya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii kuondoka haraka bungeni na kuelekea Mbarali na kesho yake Mei 12, wawe wamemfikishia taarifa nyumbani kwake.
Jana Waziri Mchengerwa alisema hakuna uporaji mifugo, watu kuumizwa wala mbuzi waliouawa kwa risasi kutokana na vurugu hizo lakini akakiri kuwa mbwa walipigwa risasi kwa sababu walikuwa wanawatishia askari kwenye kutimiza wajibu wao.
“Ni kweli askari walikwenda na helkopta katika eneo hilo, walikuta kuna ujenzi wa maboma mawili mapya, lakini watu walianza kuzuia kutiwa nguvuni kwa kutumia mawe, marungu na silaha zingine na hivyo kusababisha kitako cha bunduki kuvunjika. Nguvu waliyotumnia askari hao ilisababisha majeraha kwa watu,” amesema.
Waziri amesema katika eneo la Kijiji kichokutwa na mkasa huo, ni jirani na mahali alipouawa Askari wa Yusta Mathew (25) baada ya kutokea sintofahamu na mpishano kati ya wahifadhi na wananchi.
Kwa mujibu wa Waziri, Wizara ilitoa Sh1 milioni kila mwananchi aliyeathiriwa na majanga hayo ikiwa na lengo la kudumisha amani na mahusiano bora kati ya wahifadhi na makundi mengine.