Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yamkumbuka Mengi kwa mambo matano aliyofanya

56415 Serikali+pic

Thu, 9 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imemwelezea aliyekuwa mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi kuwa mzalendo aliyetoa mchango wake kwa Taifa katika mambo matano.

Akitoa salamu za Serikali wakati wa kuaga mwili wa mfanyabiashara huyo maarufu nchini juzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamaganda Kabudi alisema kifo cha Mengi ni pigo kubwa kwa Taifa.

Alisema wakati wa uhai wake, mfanyabiashara huyo ambaye alifariki dunia wiki iliyopita akiwa Dubai, Falme za Kiarabu, alichangia katika masuala mbalimbali aliyoyafanya kwenye elimu, afya, kilimo, madini na sekta ya uchumi kwa ujumla. “Alishiriki kuinua uwekezaji na kuboresha mazingira ya uwekezaji bila kusita kuwasaidia wawekezaji wazawa kuwekeza nchini,” alisema Profesa Kabudi.

“Aliondoka nchini akiwa mzima, lakini akiwa kule Dubai akaugua na Mungu akamchukua. Kwa muda wote Serikali kwa kushirikiana na familia ilikuwa ikifuatilia taratibu za mwili wa mpendwa wetu kurejea nchini na hilo limefanikiwa.”

Profesa Kabudi alisema mfanyabiashara huyo alitumia muda mwingi kuishauri Serikali jinsi ya kuwashirikisha wazawa na juu ya sera za kiuchumi za Taifa, akimtaja kuwa mzawa na mzalendo wa kweli aliyeishi kwenye dhana ya kuifanya Tanzania ya viwanda.

Lowassa amlilia

Jana, katika salamu zake za rambirambi, waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa alimwelezea Mengi kuwa kielelezo cha mtu aliyechukia umaskini.

Taarifa ya Lowassa iliyotolewa na Aboubakary Liongo, msaidizi binafsi wa mwanasiasa huyo, ilisema: “Dk Mengi alikuwa kielelezo halisi cha mtu anayechukia umaskini kwa vitendo na kuishi maisha yake akiwanyanyua wengine katika kuupinga umaskini.”

Alisema mfanyabiashara huyo ameacha alama kubwa ya upendo, moyo wa kutoa na unyenyekevu kwa jamii na Watanzania wataendelea kumkumbuka.



Chanzo: mwananchi.co.tz