Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yakunjua makucha kwa waajiri wasiopeleka michango kwa wakati

Katambiz Serikali yakunjua makucha kwa waajiri wasiopeleka michango kwa wakati

Thu, 29 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Tanzania imepeleka Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi Jamii bungeni wa kuwabana waajiri wasiopeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwataka kulipa kwanza michango kabla ya kuanza kusikilizwa kwa mashtaka yao mahakamani, lengo ni kuwalinda wastaafu.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Agosti 29, 2024 na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi wakati akijibu swali la Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Dk Tulia amepongeza Serikali kwa hatua waliopiga ya kushughulikia changamoto ya ucheleweshaji wa mafao ya wafanyakazi lakini akahoji ni kwanini iwekwe ndani ya siku 60, mstaafu anatakiwa awe ameshalipwa mafao yake.

”Huyu alikuwa ni mfanyakazi, kwa hiyo alikuwa anategemea mshahara mwisho wa mwezi, hii miezi miwili ambayo anachelewa kulipwa anakuwa anaishije. Lengo la mafao ina maana inachukua nafasi ya mshahara, mshahara unapokata anapaswa kupokea mafao,” amesema.

Amesema kustaafu siyo suala la dharura kwa kuwa mifuko wanakuwa wamepewa taarifa na mwajiri anafahamu hilo.

Aidha, Dk Tulia amesema changamoto ya kucheleweshwa kwa michango ya mwajiri ni jambo ambalo wameshalisema bungeni.

”Natumaini ni miongoni mwa mabadiliko mnayoleta bungeni, kwa kweli siyo kazi ya mfanyakazi kufuatilia michango kama mwajiri anapeleka ama hapeleki. Hana uwezo wa kujua wala kumfuatilia huyu mwajiri lasivyo atafukuzwa kazi kwa kweli mliangalie namna ya kulifanyia kazi,” amesema.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema siku 60 zimewekwa ndani ya kipindi hicho alipwe ili mstaafu asiweze kupata shida lakini ukweli ni kwamba analipwa wakati wowote ndani ya kipindi hicho.

Kuhusu ucheleweshaji wa michango, Katambi amesema ni Bunge liliamua kuweka riba kwa yule ambaye anachelewesha michango na wamefanya hivyo kwa sheria zinazohusiana na watumishi wa umma na binafsi.

”Moja ya marekebisho ni pamoja na huu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao tunauleta ndani ya Bunge lako tukufu. Pia kuna hatua kali tunaendelea kuchukua za kuwafikisha mahakamani,” amesema.

Amesema katika muswada huo watakuwa na pendekezo la uamuzi unaohusiana na ucheleweshaji wa michango ya wafanyakazi yafanyike baada ya mwajiri kulipa kwanza ndipo kesi ianze kusikilizwa, lengo likiwa ni kulinda hali ya wanachama wao.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Shaurimoyo (CCM), Ali Juma Mohamed amehoji Serikali ina mpango gani wa kuharakisha malipo ya wastaafu nchini.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema mpango wa Serikali uliopo kwa sasa ni kulipa wastaafu mafao ya wastaafu ndani ya siku 60 kwa mujibu wa sheria.

Amesema mpango huu umetokana na kuboreshwa kwa mifumo ya ulipaji wa mafao.

Katika swali la nyongeza mbunge huyo amehoji, Serikali haioni haja ya kurekebisha sheria ili watumishi wa Serikali wabakie katika utumishi hadi taratibu zao za mafao yao zitakapokamilika.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa mwaka 2023/24, umeshalipa mafao kwa watumishi 5016 kati ya 8,957 waliomba sawa na asilimia 54.

Amesema wastaafu hao wamelipwa ndani ya siku 60 kama sheria inavyotaka kufanya hivyo na kuwa wanaendelea kuhakikisha kuwa wastaafu 3,941 ambao hawajalipwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo waajiri kutopeleka michango, mapungufu ya kinyaraka wanalipwa.

Amesema ndani ya wiki mbili baada ya mashauri yao kufikia mwisho wa kushughulikiwa wanakuwa wamelipwa mafao yao.

Kwa upande wa wafanyakazi wa sekta binafsi, Katambi amesema kwa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) walikuwa wastaafu 3,344 walipeleka maombi ambapo kati ya hao 3,325 wameshalipwa.

Amesema idadi hiyo ni sawa na asilimia zaidi ya 90 na wote walilipwa ndani ya siku 60 tangu wastaafu.

Amesema wastaafu waliobakia hawajalipwa kwa sababu waajiri hawajapeleka michango na kesi ziko mahakamani na kuwa wanaendelea kuchukua hatua.

”Sasa hivi hakuna mstaafu anachelewa kupata mafao yake au kulipwa pensheni yake ndani ya siku 60 kwa mujibu wa sheria. Tumekuwa tukilitekeleza hilo. Na kama kuna kesi muda wote tumekuwa tukiwaomba watufikishie ofisini kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live