Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia ampongeza Hayati Magufuli kupigania JNHPP

Magu Samia Aaa.jpeg Samia ampongeza Hayati Magufuli kupigania JNHPP

Thu, 22 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema licha ya changamoto na hujuma zilizofanywa wakati wa kuanzisha mradi wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli alionyesha umahiri na ukakamavu ili kutositisha mchakato huo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Desemba 22, 2022 wakati akitoa hotuba yake, mara baada ya kulifunga rasmi geti la handaki lililojengwa kuchepusha maji ili kupisha ujenzi wa bwawa hilo lililopo Rufiji, Mkoani Pwani.

Amesema Magufuli alianzisha mradi huo licha ya changamoto na Tanzania haiwezi kuzungumzia mafanikio hayo bila ya kuwakumbuka wengine.

“Utekelezaji wa hili ulianza baada ya uhuru kipindi cha Mwalimu Nyerere, lakini wengine wote walianza kutekeleza kwa hali mbalimbali kwa uchumi mbalimbali lakini haikuwezekana kwa hali za wakati huo.

“Ilipofika awamu ya tano kwa kusukumwa na wito wa kimataifa wa kutakiwa kutengeneza umeme jadidifu unaotokaa na maji, upepo, jua na vitu vingine sisi chini ya Dk John Pombe Magufuli katika awamu ya tano tukasema liwalo na liwe, lakini adhma hii ya Mwalimu Nyerere lazima tuitekeleze.

“Nakumbuka mikiki iliyokuwepo wakati ule, hujuma zilizofanywa wakati ule lakini kwa umahiri na ukakamavu Marehemu alisema tunaendelea na tunafanya,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan pia amewahakikisha Watanzania kwamba atausimamia mradi Bwawa wa Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), hadi ukamilike.

“Wakati napewa jukumu la kuongoza nchi mradi ulikuwa asilimia 37 leo namshukuru Mungu na kupata faraja kwamba umefikia asilimia 78,” amesema Rais Samia.

Amesema JNHPP ni miongoni mwa miradi mikubwa katika bara la Afrika na Watanzania wana kila sababu ya kujivunia mradi huo wenye faida nyingi ikiwemo kuweka akiba kubwa ya maji na kuzalisha umeme hata pale ikitokea mvua imepungua.

Rais Samia amesema mradi utasaidia kudhibiti mafuriko ya mara kwa mara ya Mto Rufiji na kuwezesha kilimo cha uhakika cha umwagiliaji. Pia mradi huo utaimarisha fursa za kitalii katika eneo la kusini mwa Tanzania hasa hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kutoa ajira.

Awali, Waziri wa Nishati, Janaury Makamba amesema hatua ya kujaza maji katika Bwawa wa Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), imestahili kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku akitoa sababu tatu.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo, marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, baadhi ya wakuu wa mikoa, mawaziri, wabunge na mawaziri wa Serikali ya Misri.

Amesema miradi kama hiyo duniani inapofika hatua ya kuanza kujaza maji mijumuiko kama ya watu waliohudhuria hafla hiyo ni jambo la kawaida, muhimu na baraka.

Kabla ya kueleza hayo Makamba alimweleza Rais Samia ambaye ni mgeni rasmi kwamba, “tumeonelea kufanya shughuli ya namna hii, kwa ukubwa huu na hadhi hii kwa sababu kuu tatu, kwanza huu mradi mkubwa na wenye gharama kubwa.

“Mradi huu wa maana kubwa na jitihada kubwa za jasho na fedha za Watanzania, lakini kubwa zaidi ukikamilika utakuwa na matokeo makubwa, kwa hiyo ya kujaza maji inastahili kuhudhuriwa na kuongozwa na Rais Samia na viongozi wengine muhimu na wakubwa nchini.

Chanzo: Mwananchi