Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la Gwajima: Waziri Simbachawene awaangushia lawama DPP na DCI

AG AG Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe

Thu, 2 Sep 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi amesema azimio la Bunge la kutaka vyombo vingine vimchukulie hatua Mbunge wa Kawe (CCM) Askofu Josephat Gwajima linatosha kumfanya Mkurugenzi Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuanza uchunguzi wa shauri hilo.

Bunge liliazimia Gwajima na Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa wasimamishwe kuhudhuria vikao vya mikutano miwili ya Bunge baada ya kuwatia hatiani kwa kusema uongo, kushusha hadhi na heshima ya Bunge.

Wakati wa kuhitimisha adhabu kwa wabunge hao, Spika Job Ndugai alisema Bunge limenawa mikono kwa upande wake, hivyo kinachotakiwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Kilangi kutazama namna wanavyoweza kufanya.

Ndugai alisema kama hawatamhoji mbunge huyo, basi wasishangae kuitwa mbele ya kamati ya maadili ambayo alisema itakuwa na kauli juu yao wenyewe si kazi ya Bunge tena.

Akizungumza katika viwanja vya Bunge baada ya azimio hilo kutolewa, Profesa Kilangi alisema jambo hilo litaangukia chini ya Mkurugenzi Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa sababu ni suala la uchunguzi.

“Akishafanya uchunguzi wake atalipeleka katika hatua inayofuata ambayo ni kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP). Naye atapima kuona kama kuna jinai hapa na upo ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kuwa jinai,” alisema.

Alisema akishathibitisha kwamba kuna ushahidi wa kutosha kwa mamlaka yake atafungua kesi mahakamani.

“Lakini ni vyema kutambua mamlaka ya DPP ni mamlaka yasiyoingiliwa na taasisi yoyote, isiyoshinikizwa na taasisi yoyote, kwa hiyo na yeye atajiridhisha.Atakavyokuwa ameona na akiona kuna jinai imetendeka na ushahidi wa kutosha atalipeleka anavyoona inafaa,” alisema.

Alipoulizwa nani anakwenda kushtaki ili uchunguzi uanze, Profesa Kilangi alisema lipo azimio la Bunge linatosha kumfanya DCI kuanza uchunguzi.

Naye Waziri Simbachawene alisema maagizo ya Spika kuhusu kiongozi huyo ameyapokea, lakini hawezi kusema jambo lolote hadi atakaposhauriana na wataalamu wake.

Alisema hawakufanya haraka kumhoji Gwajima kutokana na suala hilo kuwa na mchanganyiko wa masuala ya dini.

“Ni kweli nimemsikia, lakini haya mambo yameunganisha na imani za kidini. Kabla sijasema jambo lolote lazima kwanza nijiridhishe kutoka kwa wenzangu kama tunaona iko haja ya kufanya hivyo ili tusije tukaingilia uhuru wa kuabudu,” alisema.

Hata hivyo, alisema akijiridhisha na kupata ushauri kuwa inawezekana kuhojiwa, basi watamuita na kumhoji ili kupata ukweli wa kauli zake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live