Wananchi walio wengi wamekuwa wakishindwa au kuhofia kufika ili kupata huduma katika ofisi za Umma, kutokana na uwepo wa malalamiko ya vitendo vya Rushwa ndogondogo kwa baadhi ya Watendaji Serikali wasio waaminifu.
Kauli hiyo imetolewa na WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene katika mkutano Mkuu wa mwaka wa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) unaoingia siku yake ya pili jijini Dodoma.
Amesema, “bado suala la rushwa ndogondogo ni tatizo sana kwa Wananchi wetu na huko ndiko yapo malalamiko mengi ya watu kutokana na rushwa hiyo kuwanyima fursa ya kupata huduma, jambo hili linawakera Wananchi hivyo lazima kuwa na mikakati ya kuhakikisha zinazuiliwa.”
Aidha, Simbachawene amesema ipo haja ya kutengeneza sheria za kuwashughulikia viongozi walioshiriki katika masuala ya rushwa wanapostaafu, ili kutoa funzo kwa Viongozi wengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na kupambana na Rushwa – TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, akizungumza katika mkutano huo amesema katika mwaka wa fedha uliopita taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa Shilingi 171.9 Bilioni.