Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia kufanya ziara China

Samia China Dsfc Rais Samia kufanya ziara China

Mon, 2 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika Jamhuri ya Watu wa China kuanzia tarehe 02 hadi 06 Septemba, 2024 kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation- FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing.

Aidha, wakati wa ziara hiyo Rais Dkt. Samia atakutana na mwenyeji wake Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China kwa mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano mzuri na wa kihistoria kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China ulioasisiwa miaka 60 iliyopita.

Marais hao wawili pamoja na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Hakainde Hichilema watashiriki na kushuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano ya Uboreshaji wa Reli ya TAZARA.

Pamoja na mambo mengine, miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kupewa kipaumbele kwenye Mkutano wa FOCAC ni uendelezaji wa miundombinu, kukuza uwekezaji, uendelezaji wa viwanda, kilimo cha kisasa na amani na usalama.

Rais Dkt. Samia anatarajia kuwa miongoni mwa Wakuu wa nchi watakaohutubia ufunguzi wa Mkutano wa FOCAC akizungumza kwa niaba ya Kanda ya Afrika Mashariki.

Katika ziara hii, Rais Dkt. Samia amepanga kukutana na makampuni na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji zaidi nchini Tanzania.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live