Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia: Msiwadhihaki wananchi

Samia Ikulu Leo Julai.jpeg Rais wa Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali Ikulu, Dar es Salaam

Fri, 26 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

‘Madaraka ni nguo ya kuazima.’ Huu ndiyo ujumbe alioutoa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali kufuatia mabadiliko aliyoyafanya hivi karibuni kwenye baraza la mawaziri na Serikali kwa jumla.

Katika hafla ya uapisho iliyofanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaama Rais Samia aliwaapisha mawaziri wanne, manaibu waziri wawili na makatibu tawala wawili ambapo aliwataka kutekeleza viapo vyao kwa kuwatumikia Watanzania na sio kufikiria maslahi yao binafsi.

Rais Samia amesema Serikali anayoiongoza ni ya CCM na chama hicho kinaamini binadamu wote ni sawa, hivyo amewaka viongozi hao kuheshimu utu na kuwatumikia wananchi.

“Mmeapa mbele ya Mungu mkishuhudiwa na mamlaka na wananchi. Kila mtu aende akajitafakari kwa kiapo alichokula. Kuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kama mlivyoapa, maana yake ni kuilinda Katiba na kutekeleza yake tuliyoagizwa ndani ya wa Katiba” amesema.

Uso wa kazi

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao Rais Samia ambaye uso wake jana haukuwa na tabasamu kama ambavyo amezoeleka mara kwa mara, aliwataka kutanguliza mbele masilahi ya Taifa na kuachana na mawazo ya kujinufaisha kupitia nafasi walizonazo.

Amesema: “Kwa sababu mmekula kiapo nataka niwaambie kuwa kiapo kinapiga, ukikiendea upande hakitakuacha kitakupiga. Ukikidhihaki kitakupiga kwa hiyo nendeni mkaishi na viapo vyenu.

“Kiapo mlichokula kina vifungu kadhaa na kimojawapo kinasema hautaendekeza maslahi yako binafsi kabla yale ya Taifa. Kuwa na maslahi yako binafsi kama mwanadamu ni sawa lakini yanayotakiwa kutangulia mbele ni maslahi ya Taifa.’’

Ameongeza: “Sasa wale mliozoea kutumia nafasi zenu kwa kujinufaisha, kujinyanyua nyie kabla ya Taifa naomba muache. Kama upo kwenye madaraka basi rekebisha kabla sijakuona”.

Rais Samia amesema kwa mujibu wa Katiba ibara ya 8 (1) wananchi ndiyo msingi wa mamlaka ya Serikali hivyo watendaji wanapaswa kuwatumikia wananchi na sio kuwadhihaki.

“Tuko hapa kuwatumikia wananchi. Sitarajii muende mkadhihaki wananchi au mkawadogoshe kwa sababu wao ndiyo sababu ya sisi kuwepo. Tukumbuke madaraka haya ni dhamana na inataka kufanyiwa kazi, kila mmoja awajibike kwa mwenendo, matendo na kauli njema,’’ alifafanua Samia na kuongeza:

“Waswahili wanasema madaraka haya ni nguo ya kuazima ukiitumia vizuri mwenyewe anaweza kukuvumilia lakini akibaini unakosa adabu kwa nguo yake aliyokuazima ataichukua.Niwakumbushe madaraka haya ni nguo ya kuazima saa yoyote inaweza kukuvuka. Niwaombeni twendeni tukaweke heshima kama sheria, kanuni na taratibu zetu zinavyotaka.’’

Maagizo kwa mawaziri

Mbali na maagizo hayo ya jumla, Rais Samia alikuwa na maelekezo mahsusi kwa kila wizara na watendaji wa wizara husika.

Akitoa maelekezo kwa wizara ya habari, Rais Samia alimueleza Silaa kuwa wizara hiyo muhimu katika utekelezaji wa falsafa ya 4R, hivyo ana jukumu kubwa la kusimamia uhuru wa habari na kumtaka kushirikiana na wadau katika sekta hiyo.

“Umefanya kazi nzuri ndani ya wizara ya ardhi, pamoja na mawimbi ya hapa na pale umefanya kazi nzuri na kuonesha kuwa kero za ardhi zinatatulika kupitia zile kliniki ulizokuwa unafanya.

Nenda kashirikiane na wadau wa sekta ya habari kwa kuwa ni muhimu kwa Taifa hili. Kama tunavyojenga barabara kuunganisha miji na vijiji kurahisisha mawasiliano, ndivyo hivyo tunatakiwa kuwaunganisha wananchi kwa kuwarahisishia mawasiliano,” amesema na kuongeza:

“Kuna mradi wa kujenga minara kupitia Ucsaf, nenda kahakikishe mradi unakwenda vizuri ili wananchi wapate mawasiliano ya uhakika. Nenda kasimamie agizo la kuhakikisha kufikia Disemba mifumo ya Serikali iwe inasomana, taarifa inayopita sekta moja isomeke sekta nyingine kwa zile sekta zinazoingiliana.”

Kwa Waziri Deogratius Ndejembi anayeenda Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, alielekezwa kusimama kikamilifu kutatua migogoro ya ardhi kama ambavyo alikuwa akifanya mtangulizi wake.

“Aliyeondoka kwenye wizara hii alifanya kazi nzuri, kuna hatua alizokuwa akichukua kutatua migogoro itabidi na wewe ufanye hivyo. Umefanya kazi nzuri katika kipindi kifupi kwenye wizara niliyokuweka. Ulishiriki kikamilifu kwenye suala la kikokotoo imetuweka vizuri. Kwenye ardhi nenda kaanzie pale mwenzio alipoishia” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake, Ridhiwani Kikwete ambaye ni waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, alipewa jukumu la kusimamia uratibu wa ajira kwa vijana pamoja na kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Ulikuwa naibu waziri mtiifu na bora, umefanya kazi nzuri kutokana na kazi hiyo tumeona tukupandishe. Kazi yako kubwa kwenye hii wizara ni uratibu wa kuhakikisha vijana wanapata ajira. Nataka ukawe mratibu na uhakikishe kila sekta inatoa ajira.

“Ikifika Disemba nataka uniambie tumetengeneza ajira ngapi kisekta. Ndani ya wizara yako kuna mifuko ya hifadhi ya jamii, nenda kaisimamie iendeshwe kisayansi kwa kuwa ina pesa za watu sio za Serikali. Nenda kasimamia kuhakikisha mifuko hii inakuwa endelevu na haifilisiki”amesema.

Katika maelekezo yake kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais Samia amemtaka waziri na watendaji wake, kufanya kazi kwa ufanisi kwa kile alichoeleza kuwa wizara hiyo ndiyo roho ya Serikali.

“Wizara hii ipo kwenye roho ya Serikali, upo kwenye mlango macho na masikio ya Serikali. Taswira ya nchi yetu itatoka kwenye wizara yako au kwako. Nimekuweka wasaidizi wawili, kwa bahati wote mliokwenda ni wageni wenyeji. Manaibu waziri mkamsaidie waziri maana kuna mambo mengi.

“Kama wanadamu hamkuzaliwa na baba na mama mmoja, na hata mngezaliwa hivyo mngetofautiana, kwahiyo tofauti zenu za kibinadamu zikae pembeni kazi kwanza. Muhimu kuheshimiana ndani ya wizara kila mtu ana nafasi yake. Hakuna ambaye anayajua yote ndani ya wizara lazima mshirikiane ndio muende vizuri” amesema na kuongeza.

“Moja linalolalamikiwa kwenu ni urasimu na kuwa karibu na mabalozi wa nchi nyingine, Kombo ninavyokujua wewe chakaramu unaingia kila mahali lakini sasa ingia ingia yako iwe kwa muhala.”

Neno kwa makatibu tawala

“Mmetoka ofisini sasa mnakwenda kwa wananchi na mnakwenda wakati mzuri nchi yetu imeanza vuguvugu la uchaguzi. Makatibu tawala wa mikoa ndio makamisaa mnatakiwa mkawe makini kusimamia rasilimali za Serikali na mjipange kuhakikisha mnasimamia fedha zinazoletwa huko chini zinatumika vyema kutatua kero za wananchi,”amesema Rais Samia.

Alichosema Dk Mpango

Awali akizungumza katika hafla hiyo Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliwapongeza viongozi walioapishwa na kuwataka kusimama vyema kwenye nafasi walizoaminiwa.

“Mmepewa dhamana kubwa, ni matumaini ya Rais na Watanzania kwamba mtakwenda kucheza vizuri katika nafasi zenu. “Isitokee yeyote akafikiria kwamba nafasi yake haiwezi kuzibwa, ni muhimu kuzingatia kwamba Amiri Jeshi Mkuu wakati wowote anaweza kutengeneza timu yake ili kuwaletea ushindi Watanzania,” amesema Dk Mpango.

Amewapongeza mawaziri waliopangiwa majukumu mapya, lakini akawakumbusha kuwa hakuna kazi isiyo na kasoro, hivyo muhimu wajitathmini na wasihame na changamoto walizotoka nazo katika nafasi walizokuwa nazo awali.

Walioapishwa

Mawaziri walioapishwa ni Jerry Silaa (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), Balozi Mohamed Thabit Kombo (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Deogratius Ndejembi (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Ridhiwani Kikwete (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Walemavu.

Manaibu waziri ni Cosato Chumi na Denis Londo (Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Deus Sangu anayeenda kuhudumu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Wengine walioapishwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi na makatibu tawala wawili wa mikoa ambao ni Mary Makondo (Ruvuma) na Kiseo Nzowa (Kilimanjaro).

Chanzo: Mwananchi