Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia Azindua Filamu ya ‘The Royal Tour' - Video

Video Archive
Mon, 18 Apr 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Baada ya kusubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania, Rais Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuzindua filamu ya ‘Royal Tour’ yenye lengo la kutangaza duniani vivutio vya utalii na uwekezaji vinavyopatikana hapa nchini.

Rais Samia yuko nchini Marekani kwa ziara ya kikazi na moja ya mambo atakayoyafanya huko ni kuzindua filamu ya ‘Royal Tour’ iliyorekodiwa kwenye hifadhi mbalimbali za Taifa na Mji Mkongwe huko Zanzibar.

Rais Samia Suluhu Hassan alianza kurekodi filamu hiyo Agosti 29, 2021 kwa lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii.

Wakati akirekodi filamu hiyo pamoja na mwongozaji maarufu wa filamu, Peter Greenberg, Rais Samia alitembelea na kuonyesha kwa wageni vivutio mbalimbali vya utalii, uwekezaji, sanaa na utamaduni vilivyopo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas ameandika katika ukurasa wake wa Facebook akieleza kwamba filamu hiyo itaonyeshwa kwa nyakati mbalimbali mwaka mzima kuanzia Aprili 18 mwaka huu.

“Baadhi ya TV za Marekani zitakazoonesha filamu ya ‘Royal Tour’ kwa nyakati mbalimbali kwa mwaka mzima kuanzia Aprili 18, 2022, zinaanza kutangaza ratiba zao.

“Hapa kituo cha Channel 11 (WTTW) cha mjini Chicago Illinois, moja ya vituo vikubwa katika mfumo wa utangazaji kwa umma (pbs) kinafungua mlango live Aprili 18. Kituo hiki kinaangaliwa na zaidi ya watu milioni 3.5. Orodha nyingine inakuja,” ameandika Dk Abbas.

Juzi, katika mkutano wake na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, Rais Samia alimweleza kuwa, Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji na utalii na kwamba amekwenda kuzindua filamu hiyo Marekani akiamini itaufikia ulimwengu.

“Nikiwa hapa Marekani, nitazindua kipindi cha ‘Royal Tour’, kipindi hiki kinalenga kuonyesha fursa za utalii na uwekezaji zinazopatikana Tanzania.

“Kuchaguliwa kwa Marekani kuwa sehemu ya kuzindulia, hakukuja kwa ajali, tulifanya hivyo tukitambua hapa ni mahali ambako wapenzi wa burudani na starehe wanapatikana, hiyo inafanya kuwa jukwaa sahihi la kuonyesha kipindi hiki duniani kote,” alisema Rais Samia.

Pia, alisema ana matumaini kuzinduliwa kwa filamu hiyo kutavutia watu wengi kutembelea Taifa la Tanzania katika kipindi kifupi kijacho.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz