Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Magufuli mgeni rasmi siku ya sheria nchini

1794 3 4 TZW

Tue, 23 Jan 2018 Chanzo: bongo5.com

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria itakayofanyika Februari Mosi mwaka huu.



Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma kuhusu maonyesho ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yenye maudhui ya ‘Matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili’.

“Kila mwaka Mahakama ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria ambayo huashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama, kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafunguliwa rasmi na Rais Magufuli katika viwanja vya Mahakama vilivyopo jijini Dar es Salaam,” amesema Jaji Mkuu Juma.

Jaji Mkuu amesema kuwa kabla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria, Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau muhimu katika Sekta ya Sheria watatumia siku tano kuanzia tarehe 27 hadi 31 Januari mwaka huu kwa ajili ya kufanya maonyesho yatakayotoa elimu kwa wananchi watakaopata nafasi ya kuhudhuria katika viwanja vya Mnazi Mmoja vilivyopo jijini humo.

Maonyesho hayo yatatanguliwa na matembezi maalum ya kuadhimisha Wiki ya Sheria yatakayofanyika Januari, 28 mwaka huu ambayo yataongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete yatakayoanzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mpaka viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo Rais Mstaafu Kikwete atazindua rasmi Wiki ya Sheria.

Aliongeza kuwa Wiki ya Sheria inatoa nafasi nzuri kwa wananchi kuzifahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama pamoja na wadau wa sekta ya sheria ili kufanikisha maboresho endelevu ya Mahakama.

Wadau wengine watakaoshiriki katika wiki ya sharia pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Taasisi ya Mafunzo ya Uanansheria kwa Vitendo Tanzania, Tume ya Kurekebisha Sheria, Chama cha Mawakili Tanganyika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Chanzo: bongo5.com