Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa rai kwa wawekezaji wazawa na wafanyabiashara nchini kujenga viwanda vya dawa na vifaa vya tiba hapa nchini ili kuongeza kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kukuza ajira.
Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo Jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya uzinduzi wa magari 181 yenye thamani ya shilingi bilioni 20.7 ya kusambaza dawa na vifaa vya tiba yaliyotolewa msaada na Shirika la Global Fund kwa Serikali ya Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
“Asilimia 94 ya dawa zinanunuliwa nje ya nchi, hivyo wawekezaji wazawa watumie changamoto hii kama fursa ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa hapa nchini kwetu,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alibainisha kuwa ujenzi wa viwanda hapa nchini utasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania hasa vijana pamoja na kupunguza gharama za kuagiza bidhaa nje ya nchi zikiwemo dawa na vifaa vya tiba.
Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa wataalamu na wasomi wazawa wa masuala ya afya na tiba kujiunga pamoja na kuanzisha viwanda vya dawa ili kuchochea uchumi wa viwanda na kuongeza mapato.
“Tunapoteza shilingi bilioni 500 kila mwaka kwa ajili ya kununua dawa nje ya nchi lakini tungekuwa na viwanda vyetu fedha hizo tungetumia kwenye mambo mengine ya maendeleo,” alisisitiza Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli alisisitiza kuwa madereva watakaoajiriwa kuendesha magari hayo mapya wachaguliwe kwa umakini ili kupata watu waaminifu watakaoweza kuyatunza kwa manufaa ya Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) Bw. Laurian Bwanakunu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa kutoka bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi kufikia bilioni 269 mwaka 2017/2018.