Dodoma. Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli leo Jumatatu Novemba 25, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara na Maendeleo (TDB), Admassu Tadese.
TDB imetoa mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1 (sawa na Sh2.778 Trilioni) hapa nchini na hivi sasa inakamilisha taratibu za kutoa mikopo mingine yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 500 (sawa Sh1 Trilioni 1.389) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Rais Magufuli amemshukuru Tadese kwa mchango mkubwa unaotolewa na TDB kwa maendeleo ya Tanzania bila masharti nafuu na amemuomba Tadese kuongeza mikopo zaidi itakayosaidia utekelezaji wa miradi muhimu na yenye manufaa ya muda mrefu kama vile ujenzi wa reli, mradi wa kuzalisha megawati 359 za umeme katika mto Ruhuji Mkoani Njombe na miradi ya ujenzi wa miundombinu muhimu.
Kwa upande wake, Tadese amesema TDB imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na ameelezea kufurahishwa na mazungumzo yake na Rais Magufuli ambapo ameahidi benki hiyo itazingatia ombi la kuongeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Tanzania ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway-SGR) katika kipande cha kuanzia Dodoma kuelekea Kanda ya Ziwa na kanda ya Magharibi ambako itaunganisha na nchi jirani zisizokuwa na bahari.
Amempongeza Rais Magufuli kwa jinsi anavyosimamia uchumi wa Tanzania na kubainisha kuwa ukuaji mzuri wa uchumi ni jambo linaloivutia benki hiyo kushirikiana zaidi na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Doto James.