Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli leo February 4, 2018 amehudhuria Ibada ya kuwekwa wakfu Askofu wa Tano wa Dayosisi ya Dar es Salaam Askofu Jackson Sosthenes Jackson katika Kanisa kuu la Mtakatifu Albano Upanga.
Rais Magufuli amewataka viongozi na waumini wa madhehebu ya dini nchini kujiepusha na migogoro ambayo imekuwa ikiharibu sifa na heshima ya taasisi hizo muhimu katika jamii.
JPM amesema viongozi wa Serikali husikitishwa na uwepo wa migogoro katika madhehebu ya dini, na hupata mashaka kama kweli viongozi wa madhehebu husika wanazingatia matakwa ya Uchungaji.
Amempongeza Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dr. Jacob Chimeledya kwa kuumaliza mgogoro uliokuwa ukilikabili Kanisa hilo na hatimaye kufikia hatua ya kumweka wakfu Askofu Jackson Sosthenes Jackson kuwa Askofu wa Tano wa Dayosisi ya Dar es Salaam.
Rais Magufuli amemtaka Askofu Jackson SosthenesĀ kuwa Askofu wa wote, kuvunja makundi yaliyokuwepo katika Dayosisi hiyo, kutolipiza kisasi na kusamehe yote yaliyopita na badala yake ajenge Dayosisi imara na aongoze kwa haki na upendo kwa wote.
Pia JPM amewahakikishia viongozi wa Kanisa la Anglikana Tanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kushirikiana na kanisa hilo na madhehebu mengine ya dini katika shughuli zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za kijamii kama vile hospitali, na shule.
Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Ackson Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya TatuĀ Benjamin William Mkapa na Mkewe Mama Anna Mkapa na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.
LIVE: JPM KWENYE SHEREHE ZA KUMUWEKA WAKFU ASKOFU JACKSON SOSTHENESI, BONYEZA PLAY HAPA CHINI KUTAZAMA