Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ameendesha harambee kwa ajili ya kuchangia ununuzi wa Bajaji ya Nyangoma James ambaye ni mlemavu na mkazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Harambee hiyo ameiendesha leo Juni 19, 2020, wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Ubungo, wakati akirejea Dar es Salaam akitokea Dodoma, ambapo katika harambee hiyo Rais Magufuli yeye ametoa kiasi cha Shilingi Milioni 5, huku harambee hiyo akikusanya Mil 3.7.
Awali Rais Magufuli amewapongeza wakazi wa Ubungo kwa kupata mradi wa ujenzi wa barabara za juu, na kwamba Serikali ya awamu ya Tano imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 210 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo na kwa ajili ya ujenzi wa barabara zingine za njia nane kwa kuwa imedhamiria kuibadilisha Tanzania.