Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Tanga: Madiwani waadabisheni wakuu wa idara

Video Archive
Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Handeni. Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martin Shigela amewaagiza madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Handeni, kuwachukulia hatua  za kinidhamu wakuu wa idara ambao wanakiuka maadili ya kazi.

Shigela ametoa agizo hilo leo Julai 3 wakati wa kikao maalum cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG) kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Amesema kuwa hakuna sababu ya kuendelea kulea watu ambao wanakiuka miiko ya kazi zao kwa kufanya makosa kwa makusudi, hao wasivumiliwe na badala yake wachukuliwe hatua.

Shigela ameongeza: “Waheshimiwa madiwani mna uwezo wa kumchukulia hatua mkuu wa idara ambaye anakiuka taratibu, kama anavyochukua hatua Rais wetu na sisi kwa nafasi zetu tunaweza kufanya hivyo.”

Mbunge wa Jimbo la Handeni Vijijini, Mboni Mhita amemtaka, mkurugenzi pamoja na timu yake kuhakikisha wanatosha kwenye nafasi zao kwa kufanya kazi kwa uhakika.

Amesema hakuna sababu ya kuelekezana kila siku wakati kila mmoja anafahamu wajibu wake, hivyo kila mwenye makosa aadhibiwe.

Ofisa mkaguzi wa nje, ofisi ya taifa ya ukaguzi mkoa wa Tanga Ahmad Mfaume amesema ili kufutiwa hoja zenye mashaka halmashauri zinatakiwa kupeleka vielelezo vya hoja hizo mapema ofisini kwake.

Amesema katika baadhi ya hoja wahusika wamesema vielelezo vyao vipo, hivyo ni vizuri kuviwahisha mapema.

Mkurugenzi mtendaji halmshaauri ya wilaya ya Handeni, William Makufwe amesema wameashaanza kuwachukulia hatua watumishi ambao wameonekana kukiuka maadili ya kazi.

Katika ukaguzi huo wa CAG, halmashauri ya wilaya ya Handeni imepata hati yenye mashaka huku halmashauri ya mji wa Handeni ikipata hati safi.

Chanzo: mwananchi.co.tz