Kocha wa Manchester City, Pep Gaurdiola amesisitiza kwamba hawana haraka sana ya kusajili katika dirisha hili licha ya wapinzani wao kuonekana wako bize sokoni.
Man City ambayo hivi karibuni iliripotiwa kufanya makubaliano na Atletico Madrid kwa ajili ya kuwauzia Julian Alvarez kwa Pauni 82 milioni, hadi sasa imefanya usajili wa mchezaji mmoja tu.
Kwa mujibu wa Guardiola, moja kati ya maeneo ambayo wanaweza kusajili ni kiungo mkabaji ambaye atakuwa na uwezo wa kucheza kama beki wa kati.
Guardiola anataka kiungo ambaye ataenda kuwasaida Rodri na Mateo Kovacic lakini amesisitiza kwamba hata kama watasajili basi haitakuwa kwa kutoa pesa nyingi.
“Ndio, tutaona, ikiwa tunamhitaji mchezaji yeyote, pesa tutakayotoa itatakiwa kuwa sahihi, kuhusu kuuza inabidi tusubiri hadi kufikia mwisho wa dirisha,” alisema Guardiola.
“Kuhusu kusajili labda tunaweza kuchukua kiungo mkabaji anayeweza kucheza beki wa kati au beki wa kati anayeweza kucheza katika nafasi ya Rodri.”
Alipoulizwa maoni yake juu ya usajili unaofanywa na Arsenal na Man United katika dirisha hili Guardiola kama amepata wasiwasi wowote alisema: “Kwa miaka mingi wamekuwa wakifanya hivyo, wala husikii ikizungumziwa, inakuwa habari ya kupita mara moja tu, ila shida inakuja pale Man City ikitoa pesa nyingi.”
Guardiola pia anasema kuelekea msimu ujao itakuwa sio rahisi kwao kushinda ubingwa moja kwa moja kwa sababu wachezaji wengi wameshashinda tayari hivyo hawawezi kuwa na njaa na shauku ya kutaka kushinda tena, hivyo lengo ni kumpambania kila mchezaji aimarishe kiwango chake.