Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nape, Makamba wameenguliwa na haya

Nape, Makamba Watumbuliwa.png Wadau: Nape, Makamba wameenguliwa na haya

Tue, 23 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mjadala mkali umeibuka kwenye mitandao ya kijamii baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, wengi wakihoji kilichowaondoa mawaziri Nape Nnauye na January Makamba.

Wachambuzi wa siasa wamesema kilichofanywa na Rais Samia ni mabadiliko ya kawaida kwa kuwa ni suala la uwajibikaji, huku wengine wakihusisha na kauli za hivi karibuni za mmoja wa mawaziri hao.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, Rais amefanya mabadiliko ili kuboresha na kulisuka vyema Baraza la Mawaziri kuleta tija kwa Watanzania. Waliondolewa na kuzua mjadala ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Pia yuko Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato, Mbunge wa Bukoba Mjini. Licha ya Rais kutoeleza sababu za kutengua nafasi za mawaziri hao, baadhi ya watu walionesha kufurahia kuondolewa kwa Nape, wakielezwa kuchukizwa na kauli yake ya hivi karibuni kuhusu uchaguzi, waliyoitafsiri kukwaza ustawi wa demokrasia nchini. 

Nape alisema kwamba matokeo ya uchaguzi hayategemei sanduku la kura bali nani anasimamamia uchaguzi na kuhesabu kura. Safari ya uwaziri ya Nape ilianzia mwaka 2016, alipoteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kudumu kwa muda mfupi, aliondolewa Julai 22, 2017.

Januari 8, 2022, Rais Samia alimrudisha Nape kwenye nafasi hiyo akiwa Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hadi juzi usiku alipomtengua.  January alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia mwaka 2012 na kuitumikia nafasi hiyo kwa miaka mitatu hadi 2015.

Mwaka 2016, aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira na kisha kumwondoa katika nafasi hiyo Julai 21, 2019.

Septemba 2021, Rais Samia alimteua kuwa Waziri wa Madini na August 30, 2023 akamhamisha kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki hadi juzi usiku. Tangu mwaka 2010, January ni Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema alisema jana kuwa alitegemea viongozi hao, hasa Nape kuondolewa katika nyadhifa zao kutokana na kauli zao.

Alisema kauli ya Nape ya ‘goli la mkono’ ni hatari kwa nchi hiyo inayozingatia misingi ya kidemokrasia na uchaguzi huru, inatoa taswira ya kuwa kuwa hakuna demokrasia imara katika nchi.

Alisema demokrasia ndio njia pekee ya wananchi kuiondoa serikali iliyopo madarakani kama wakiona haifanyi vizuri, hivyo kauli hiyo inavua dhana hiyo iliyojengeka katika mawazo ya wananchi.

"Nape ni sehemu ya baraza la mawaziri, kutoa kauli kama ile ni hatari sana kwa demokrasia, serikali ni lazima ijenge taswira ya nchi kutegemea uchaguzi salama na wa haki," alisema Lema.

Mwanasiasa huyo pia alisema hakushangazwa kuondolewa kwa January kwa kuwa alitegemea kuona baadhi ya mawaziri wakitolewa, akitabiri hali hiyo pia kwa Waziri mteule wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) - Shule Kuu ya Elimu, Dk. George Kahangwa alisema kilichotokea kwa viongozi hao kilitarajiwa na kuwa Nape alipaswa ajiuzulu mwenyewe kutokana na kauli aliyoitoa hivi karibuni kuhusu mshindi katika uchaguzi.

Kuhusu viongozi wengine waliotenguliwa, Kahangwa alisema ni kawaida kwa kuwa kiongozi anapoona wasaidizi wake hawaendani na kasi anayoitaka, anawajibika kuwaondoa na kuweka wengine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, alisema alichokifanya Rais Samia ni alama ya uwajibikaji na uwajibishaji. Juzi usiku, Rais Samia alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.

Mbali na mawaziri hao, Silaa ameteuliwa kushika nafasi ya Nape, huku nafasi yake ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikichukuliwa na Deogratius Ndejembi ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Rais Samia pia amemteua Ridhiwani Kikwete kuwa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). Kabla ya uteuzi huo, Ridhiwani alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Pia Rais amemteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Balozi wa Tanzania Italia. 

Vilevile, Rais Samia amemteua Cosato David Chumi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akichukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa atapangiwa kituo cha kazi.

Saa chache kabla ya taarifa ya uteuzi mpya wa Rais Samia kutangazwa, Ofisi ya Bunge ilitoa taarifa kwa umma kuwa Balozi Mbarouk amemwandikia Spika barua kuomba kujiuzulu ubunge wa kuteuliwa na Rais.

Rais pia ameteua Deus Sangu kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, huku akimteua Dennis Londo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

Taarifa ya Ikulu pia ilieleza kuwa Rais amemteua Eliakim Maswi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), huku akimteua Mary Makondo kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma. Kabla ya uteuzi alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, anachukua nafasi ya Rehema Madenge ambaye amestaafu.

Kiseo Nzowa ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro. Kabla ya uteuzi alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu, huku Musa Haji Ali akiteuliwa kuwa Balozi. Kabla ya uteuzi alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu.

Rais Samia amemteua Louis Bura kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato akichukua nafasi ya Said Nkumba ambaye amepangiwa majukumu mengine, huku Kemirembe Lwota akihamishwa kutoka Wilaya ya Manyoni kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti.

Dk. Vincent Mashinji amehamishwa kutoka Wilaya ya Serengeti kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya Manyoni, huku Dk. Maulid Madeni akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Afraha Hassan amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, akichukua nafasi ya William Mwakalambile ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Rais amemteua Dennis Simba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PPRA. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live