Mtoto Asimwe Novarti mwenye ulemavu wa ngozi (Albino) aliyeibwa Mei 30 mwaka huu nyumbani kwao na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Mbale, amekutwa ameuawa na kisha mwili wake kufungwa kwenye sandarusi na kutelekezwa kwenye moja ya karavati iliyopo Barabara ya Ruhanga Makongara, Kata ya Ruhanga, Tarafa ya Kamachumu wilayani Muleba huku baadhi ya viungo vya mwili wake vikikosekana.
Kwa mujibu wa Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba, Benjamin Richard Mwikasyege amesema, baada ya kuripotiwa kuonekana kwa mfuko uliokuwa umefungwa mwili wa mtoto huyo, wamekuta baadhi ya viungo vya mwili wake havipo na kwasasa mwili huo umechukuliwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi.
Mtoto Asimwe Novarti aliyekuwa na miaka miwili aliibwa nyumbani kwao na watu wasiojulikana ambao walifika nyumba kwa mtoto huyo na kujifanya wanahitaji msaada kutoka kwa mama wa familia hiyo ambaye baada ya kutoka ndani ili kutoa msaada walimkaba na kisha kutokomea na mtoto huyo.