Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili wa Mengi kuletwa leo, maandalizi yaanza Machame

55836 Pic+mwili+%253Dmengi

Mon, 6 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Hai. Wakati mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi ukiletwa mchana wa leo, maandalizi kijijini kwake Nkuu, Machame mkoani Kilimanjaro atakapozikwa yameanza.

Maandalizi hayo ni pamoja na kupaka rangi baadhi ya maeneo, kuandaa mfumo wa mawasiliano, maturubai pamoja na viti.

Mengi aliyezaliwa Mei 29, 1942, alifikwa na mauti usiku wa kuamkia Mei 2 akiwa Dubai, Falme za Kiarabu na mwili wake unatarajiwa kuletwa saa nane mchana na Shirika la Ndege la Emirates.

Jana, mshehereshaji katika msiba huo, Nassa Kingo aliwaambia waombolezaji mbalimbali waliokuwa nyumbani kwa marehemu, Kinondoni, Dar es Salaam kuwa mara baada ya mwili wa mfanyabiashara huyo mmiliki wa vyombo vya habari vya ITV/Redio One na The Guardian Limited kuletwa, utapitishwa katika maeneo ya Tazara, Buguruni, Ilala, Kigogo, Magomeni, Kinondoni, Morocco, kisha kuingia Barabara ya New Bagamoyo.

“Utapita eneo la Makumbusho, Sayansi, Mwenge hadi Hospitali ya Lugalo utakapohifadhiwa,” alisema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa Ijumaa iliyopita na msemaji wa familia, Michael Ngalo, kesho mwili wa Mengi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), utaangwa kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na baada ya hapo utapelekwa nyumbani kwake Kinondoni na keshokutwa utasafirishwa kwenda Machame kwa mazishi yatakayofanyika Alhamisi.

Habari zinazohusiana na hii

Wageni mbalimbali jana walifika nyumbani kwa Mengi kutoa salamu za pole. Miongoni mwao ni Mama Salma Kikwete, mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, mawaziri, January Makamba (Muungano na Mazingira), Doto Biteko (Madini), wabunge Nape Nnauye (Mtama) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini).

Mama Salma alisema Mengi ameacha pengo kubwa na atakumbukwa kwa mambo mbalimbali ikiwamo kujitolea kuwasaidia wanafunzi wanaosoma katika shule za sekondari zinazomilikiwa na Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake (Wama).

Makamba alisema Taifa lina msiba mzito kwa kumpoteza mdau muhimu kwenye sekta ya mazingira huku Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala akisema idara hiyo imepata pigo kwa kumpoteza mdau mkubwa.

Nape alisema Mengi ni mmoja kati ya watu waliotoa mchango mkubwa kwenye masuala ya siasa na kifo chake kimeacha alama kubwa huku Zitto akisema msiba huo ni mzito kutokana na mchango mkubwa ambao aliutoa kwa jamii.

Imeandikwa na Bakari Kiango, Fortune Francis (Dar) na Janeth Joseph.



Chanzo: mwananchi.co.tz