RAIS wa Uganda Yoweri Museveni ameipongeza Tanzania kuingia uchumi wa kati na kusema kuwa Uganda ipo njiani kuifuata.
Rais Museveni ameyasema hayo muda mfupi baada ya kushuhudia kiapo cha Rais John Magufuli mjini Dodoma leo.
“Miezi mitatu imepita tumesikia mmeingia uchumi wa kati, niwapongeze sana kwa hilo, kutoka kwenye kuomba, kisha kuingia kwenye ustawi, uzalishaji mali na bidhaa na sisi tutafuata nyayo,”amesema na kuongeza
“Waganda walikuwa wamelala usingizi, waligubikwa na uakabila, udini, sasa ndio wameanza kuamka, sijui hapa Tanzania lakini Uganda kati ya watu 100, 32 ndio wanaozalisha mali na ndio nguvu kazi, walioibaki wanafanyia kazi tumbo,” alieleza Museveni.
Hata hivyo amesema kwasasa raia wa Uganda wameanza kuamka na kwamba uzalishaji umeongezeka.
“Tuna maziwa, ndizi, sukari na malighafi zingine za viwanda. Nakuomba Rais Magufuli nikuletee sukari, soko letu la ndani halitoshi tunafikiria kuuza Tanzania, kwa nchi za SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) na COMESA (Jumuiya ya soko la pamoja la nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika),”amesema Museveni
Kauli ya Museveni inakuja miezi kadhaa baada ya Benki ya Dunia kuitangaza Tanzania kuingia nchi ya uchumi wa kati.